YANGA HAWATOKI JUMAMOSI- MTIBWA SUGAR

Uongozi wa Mtibwa Sugar umesema hautishwi na kipigo cha 3-0 ambacho Yanga imekitoa kwa Azam FC 3-0 kabla ya mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu huu itakayozikutanisha kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro Jumamosi.

Ikitoka kushiriki michuano ya Kombe la Kagame, Azam FC ilikubali kichapo hicho dhidi ya kikosi cha Yanga kinachonolewa na kocha wa zamani wa timu ya Taifa (Taifa Stars) katika mechi ya Ngao ya Jamii iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumapili.


Kocha Mkuu wa Mtibwa Sugar, Mecky Mexime, jana alizungumza kwa njia ya simu kutoka Manungu, Morogoro kuwa kikosi chake kimejiandaa vema na mchezo huo na anaamini ataendeleza rekodi yake nzuri kila anapokutana na Yanga kutokana na kuzijua mbinu za kocha wao.

Maxime alisema hana wachezaji wenye majina 'makubwa' lakini wana uwezo wa kuikabili Yanga na timu nyingine kwenye ligi hiyo ambayo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kuanzia mechi ya kwanza hadi ya mwisho wa msimu.

Alisema Yanga inatakiwa kujipanga na kujiandaa kwa sababu mechi hiyo haitakuwa na 'mteremko'.

Aliwataka waamuzi watakaopewa nafasi kuchezesha mechi hiyo kuwa waadilifu kwa kufuata sheria 17 za mchezo huo ili mshindi atakayepatikana awe ni wa haki bila ya malalamiko ya upande wowote.

"Tunaendelea na maandalizi kama programu yetu tulivyoiandaa, kwetu mechi hiyo ni ya kawaida, hatuiwazii kama ambavyo wao wanatufikiria, huyo Jaja (Genilson) akifika Morogoro atakuwa 'Jojo', alisema Mexime.

Aliongeza kuwa anafahamu mbinu za Kocha Mkuu wa Yanga, Mbrazil, Marcio Maximo, hivyo kwake amekuwa na kazi nyepesi kuwaandaa wachezaji wake jinsi ya kuwakaba nyota wa Yanga.

"Najivunia wachezaji wangu, wengine wapya tumesajili kutoka Ligi Daraja la Kwanza lakini wanauwezo na wataonyesha kuwa Tanzania ina vipaji na klabu zisikimbilie kusajili wageni," aliongeza nahodha huyo wa zamani wa timu ya Taifa (Taifa Stars) ambaye pia aliwahi kuwa chini ya Maximo.

Mbrazil huyo amejerea nchini na kupewa mkataba wa miaka miwili akirithi mikoba ya Mholanzi Hans van Pluijm, ambaye aliondoka Yanga baada ya kupata kazi Saudi Arabia.

Kwa miaka mitano sasa Yanga haijawahi kushinda dhidi ya Mtibwa kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro huku timu hiyo inayonolewa na nahodha wake wa zamani na Taifa Stars, Mexime ikiwa ni moja ya timu zilizoipoteza maboya Yanga katika harakati zake za kutetea taji la VPL msimu uliopita iliyoupoteza kwa Azam FC.

Mara tu baada ya mechi yao dhidi ya Azam, Maximo alisema kikosi chake ambacho jana kilirejea tena kambini baada ya kupata mapumziko ya siku moja, kitakuwa na wakati mgumu dhidi ya Mtibwa Jumamosi.

"Nimeelezwa kwamba Yanga haijawahi kuifunga Mtibwa kwa muda mrefu nje ya Dar es Salaam. Jumamosi itakuwa mechi nzuri na ngumu kwa sababu Mecky (Mexime) anazifahamu mbinu zangu kwa kiasi kikubwa maana alikuwa nahodha wangu Taifa Stars," alisema Maximo.

Mtibwa ambao hawajawahi kutwaa ubingwa wa VPL tangu wautwae kwa mara ya mwisho mara mbili mfululizo 1999 na katika mwaka wa mabadiliko ya karne, wamekuwa wakionesha upinzani mkali kwenye Uwanja wa Jamhuri wanapocheza dhidi ya timu kongwe na zenye mashabiki lukuki nchini, Simba na Yanga.

Timu hiyo inayomilikiwa na kiwanda cha sukari cha Mtibwa Sugar chenye maskani yake Manungu, Turiani nje kidogo mwa mji wa Morogoro, imekuwa ikisifika kwa kuibua vijana wengi wenye vipaji ambao hata hivyo huwa haidumu nao kwa kipindi kirefu kabla hawajachukuliwa na Simba na Yanga.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA