SIMBA YAKWAA KISIKI KWA OKWI TFF

Huku ikiwa tayari imewasilisha madai ya Dola 500,000 za Marekani, uongozi wa klabu ya Yanga jana uliwasilisha pingamizi rasmi dhidi ya mshambuliaji Emmanuel Okwi, ambaye Simba ilitangaza kumsajili.

Katika malalamiko ya awali, Yanga pia imeomba Simba ifungiwe kwa kukiuka taratibu huku pia mshambuliaji huyo wa timu ya Taifa ya Uganda (Uganda Cranes) afungiwe kucheza soka.

Habari ambazo zimepatikana jijini Dar es Salaam zinaeleza kuwa Yanga iliwasilisha pingamizi hilo katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ikieleza kwamba Okwi bado ni mchezaji wake halali.


Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Simba ndiyo klabu iliyowekewa pingamizi nyingi zaidi ukilinganisha na klabu nyingine zinazoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakayofanyika kuanzia Septemba 20 mwaka huu.

Mbali na Okwi, baadhi ya nyota wengine waliowekewa pingamizi wa Simba ni pamoja na Abdi Banda ambaye ametoka Coastal Union ya Tanga na Shafii Hassan wa Zimamoto ya Unguja, Zanzibar.

"Jumamosi ndiyo majina ya wachezaji waliopitishwa kucheza yatabandikwa rasmi," alisema kiongozi mmoja wa TFF ambaye hakutaka jina lake litajwe.

Katibu Mkuu wa TFF, Selestine Mwesigwa, jana hakuweza kupatikana kueleza ni wachezaji wangapi wamewekewa pingamizi na klabu zao za zamani.

Wachezaji ambao hawatapitishwa kwenye mchakato huo wa usajili, hawatazitumikia klabu zao katika msimu mpya wa ligi mpaka pale taratibu za usajili wao zitakapokamilika.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA