MASIKINI SIMBA! KIONGERA KUIKOSA YANGA OKTOBA 12

MSHAMBULIAJI Mkenya, Paul Raphael Kiongera anaweza kuukosa mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wapinzani wa jadi, Yanga SC Oktoba 12, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hiyo inafuatia kuumia katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Jumapili Uwanja wa Taifa, Simba SC ikilazimishwa sare ya 2-2 na Coastal Union, licha ya kuongoza kwa 2-0 hadi mapumziko.

Kiongera alitokea benchi dakika ya 67, lakini dakika mbili kabla ya filimbi ya mwisho akampisha Amri Kiemba baada ya kuumia, kufuatia kugongana na kipa wa Coastal Union, Shaaban Kado.


Kiongera ameumia goti na leo alikuwa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili kufanyiwa vipimo, ila inasemekana mchezaji huyo ana maumivu sugu ya goti hilo baada ya kuumia awali kwao, Kenya.

Taarifa za awali zinasema Kiongera anaweza kuwa nje ya Uwanja kwa muda wa kati ya wiki sita hadi miezi miwili kabla ya kuanza mazoezi mepesi, maana yake hataweza kucheza Oktoba 12 pambano la watani.

Tayari kuna hali ya wasiwasi ndani ya Simba SC kwamba huenda ‘wameingia mkenge’ kumsajili Mkenya huyo bila kumfanyia vipimo vya afya, kufuatia habari kwamba ana maumivu sugu ya goti.

Kiongera aliumia baada ya kugongana na kipa wa Coastal, Shaaban Kado

Majeruhi wengine wa Simba SC beki wa kushoto Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ aliyeumia nyama wiki mbili zilizopita mazoezini yuko katika wiki ya mwisho ya mapumziko, wakati winga Haroun Chanongo aliyeumia goti Jumapili pia dhidi ya Coastal, atakuwa nje kwa siku nne tu.

Habari njema zaidi kwa wana Simba SC ni kwamba, kiungo ‘mchapakazi’ Jonas Gerald Mkude yuko fiti kwa asilimia 100 na Dk Yassin Gembe amesema anaweza kuanza kucheza hata Jumamosi dhidi ya Polisi Morogoro.

“Ni uamuzi wa kocha tu, lakini ukweli ni kwamba Mkude yuko fiti kabia sasa na anaweza kuanza kucheza, uzuri ni kwamba pamoja na kuwa nje kwa muda mrefu, lakini hajaongezeka uzito,”amesema Gembe leo.

Baada ya sare ya 2-2 juzi na Coastal, Simba SC iliondoka Dar es Salaam jana jioni kurejea Zanzibar kwenye kambi yake.

Wekundu hao wa Msimbazi, watashuka tena dimbani Jumamosi kumenyana na Polisi Morogoro iliyofungwa 3-1 na Azam FC katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu.



Chanzo Bin Zubeiry

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA