MAKALA: SIMBA IMEBUGI KWA DONALD MOSOTI

Na Prince Hoza

LIGI kuu ya Vodacom Tanzania bara (VPL) ilianza rasmi mwishoni mwa wiki iliyopita ambapo karibu timu zote zilishuka dimbani siku ya jumamosi na jumapili, ufunguzi huo wa ligi ulianza jumamosi na siku ya jumapili kulichezwa mechi moja tu.

Mabingwa wa zamani wa Tanzania bara Simba SC walishuka dimbani kukabiliana na mabingwa wa bara mwaka 1989 Coastal Union ya Tanga kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo timu zote mbili zilitoshana nguvu kwa kutoka sare ya kufungana mabao 2-2, Simba ikiutumia uwanja wake wa nyumbani ilianza vema kipindi cha kwanza kwa kufanikiwa kujipatia mabao yake mawili.

Mabao ya Simba yaliwekwa kimiani na Shaaban Kisiga 'Marone' na Amissi Tambwe, magoli yote mawili yalitokana na juhudi binafsi za kiungo mshambuliaji raia wa Uganda Emmanuel Okwi ambaye aliweza kupiga krosi iliyomkuta Tambwe na kuweka mpira kimiani.


Na goli la kwanza kazi nzuri ya Okwi ilisababisha adhabu ndogo ambapo mfungaji aliweza kumtungua kipa wa Coastal Union Shaaban Hassan Kado.

Hata hivyo Coastal Union walisawazisha mabao yote mawili katika kipindi cha pili, uzembe wa mabeki wa Simba kutegea offside ulipelekea mfungaji Mkenya Lutimba Yayo Kato kumfunga kirahisi kipa Ivo Mapunda.

Naye Mkenya mwingine Rama Salim aliweza kuisawazishia timu yake ya Coastal Union na kufanya matokeo yasomeke 2-2, matokeo hayo yamewasononesha mashabiki wa Simba ambao tayari walishaanza kusherehekea kalamu ya mabao katika mchezo huo.

Tatizo kubwa lilioonekana katika timu ya Simba ni ukosefu wa beki ya kati hasa baada ya kumtema katika dakika za mwisho mlinzi ngongoti Donald Mosoti, naweza kusema lilikuwa kosa kubwa sana kwa klabu ya Simba kulifanya msimu huu.

Huwezi kumtoa beki na kumleta kiungo mshambuliaji wakati tayari klabu hiyo inao viungo wengi wenye uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za magoli, baadhi ya mashabiki ambao walichukizwa na matokeo hayo waliweza kuzungumza na Gazeti hili na kudai umuhimu wa Mosoti umeonekana.

Mashabiki hao wamedai Mosoti alikuwa na umuhimu mkubwa katika kikosi cha Simba hasa kutokana na mchango wake awapo katika nafasi yake na amekuwa akimsaidia vizuri nahodha wa timu hiyo Mganda Joseph Owino.

Mozoti alisajiliwa wakati wa usajili wa dirisha dogo mwaka jana akiwa sambamba na mlinda lango Ivo Mapunda wote wawili walikuwa wachezaji wa Gor Mahia ya Kenya.

Uwezo wake ulijidhihirisha katika mchezo wa Nani mtani wa Jembe baina ya Yanga na Simba uliochezwa Desemba 21 mwaka jana kwenye uwanja wa Taifa ambapo Simba iliilaza Yanga mabao 3-1.

Anamwaga wino: beki kisiki Donald Mosoti raia wa Kenya anamwaga wino katika klabu ya Simba huku pembeni yake ni aliyekuwa katibu wa kuajiliwa wa klabu hiyo Evodies Mtawala, wote hawa kwa sasa wapo nje ya klabu hiyo

Katika mchezo huo ambapo Simba ilikuwa ikinolowa na Mcroatia Zdravko Logarusic huku Yanga ikinolewa na Mholanzi Ernie Brandts na msaidizi wake Fred Minziro, Mosoti alionyesha kiwango cha hatari na kuwafurahisha mashabiki wa Simba waliofurika uwanjani hapo.

Tatizo kubwa lililokuwa likiigharimu Simba kwa kipindi kirefu tangia alipoondoka mlinzi wake Kelvin Yondani aliyetimkia Yanga kulisababisha furaha ipotee na kuiofanya Simba ipoteze heshima yake.

Kutua kwa Mkenya huyo ngongoti na Mganda Owino kuliweza kurejesha imani kwa mashabiki wake, Simba ilimaliza ligi katika nafasi ya nne, msimu mpya ukiwa tayari kuanza Simba ilimfuta kazi kocha wake Logarusic na kumuajili aliyekuwa kocha wake wa zamani Mzambia Patrick Phiri.

Kutua kwa Phiri katika kikosi hicho kuliendana na mabadiliko kadhaa katika kikosi chake, viongozi wa Simba waliingia katika mgogoro mwingine na watani zao Yanga ambapo walitangaza kumchukua Emmanuel Okwi ambaye alikuwa na mkataba na Yanga wa miaka miwili na nusu.

Kutua kwa Okwi Simba kulipelekea kukata jina la mchezaji mmoja wa kigeni, tayari Simba ilikuwa na wachezaji watano wa kigeni ambao ni Pierre Kwizera, Raphael Kiongera, Amissi Tambwe, Joseph Owino na Donald Mosoti.

Hivyo kuongezeka kwa Mganda Emmanuel Okwi kumefanya idadi ya wachezaji wa kigeni kuongezeka na kuwa sita ambapo ni kinyume na taratibu za TFF inayoagiza kila klabu kuwa na wachezaji watano wa kigeni.

Beki mkabaji Donald Mosoti aliyevaa uzi wa rangi ya bluu akimdhibiti mshambuliaji wa timu pinzani katika ligi kuu ya Kenya, Mosoti alijiunga na Simba ya Tanzania lakini imemchinjia baharini katika dakika za mwisho

Hatimaye Okwi alichukua nafasi ya beki mahiri Donald Mosoti, pengo la Mosoti mpaka sasa halijaweza kuzibwa huku hofu ikizidi kutanda wakati timu inaelekea kwenye mechi ngumu za ligi kuu.

Ni kosa kubwa lilifanyika, tayari Simba inao viungo wengi wenye uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za kufunga, pia inao washambuliaji wengi wenye uwezo wa kufunga, kulikuwa hakuna umuhimu wa kumwondoa beki tegemeo kama Mosoti, cha kufanya sasa kocha Phiri atalazimika kutengeneza safu mpya ya ulinzi ili angalau iweze kufika hadi wakati wa usajili wa dirisha dogo, tuonane wiki ijayo.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA