COASTAL UNION YAISHIKA SHARUBU SIMBA UWANJA WA TAIFA

Simba ilipoteza uongozi wake wa magoli mawili na kujikuta ikilazimishwa sare ya 2-2 dhidi ya 'ndugu zao' wa Coastal Union ya Tanga katika mechi yao ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana.

Ikionekana kudhamiria kuwa na matokeo tofauti na ya mahasimu wao Yanga ambao juzi walikumbana na kipigo cha 2-0 dhidi ya Mtibwa Sugar mjini Morogoro, Simba walihitaji dakika sita tu za kwanza kupata bao la kwanza.

Mchezaji mpya Shabani Kisiga aliifungia Simba goli la kuongoza kwa 'fri-kiki' tamu iliyokwenda moja kwa moja wavuni. Refa Jacob Adongo aliamuru adhabu hiyo baada ya Emmanuel Okwi kukwatuliwa na Selemani Rajab nje kidogo ya boksi la Coastal.


Mfungaji bora wa msimu uliopita, Mrundfi Amissi Tambwe aliifungia Simba goli la pili katika dakika ya 36 kwa kichwa akimalizia krosi safi ya Emmanuel Okwi, aliyerejea Msimbazi baada ya msimu uliopita kuitumikia Yanga kwa muda mfupi.

Coastal walirejea kipindi cha pili kwa kuwaingiza Lutimba Yayo na Ayoub Yahaya wakichukua nafasi za Selemani Rajab na Razak Khalfan, mabadiliko yaliyokuwa na manufaa kwa wageni hao.

Yayo aliifungia Coastal goli la kwanza katika dakika ya 66 kwa shuti kali la kustukiza lililomshinda kipa wa Simba, Ivo Mapunda na zikiwa zimesalia dakika tisa mechi kumalizika Rama Salim aliwashangaza wenyeji kwa goli la 'fri-kiki' iliyokwenda moja kwa moja wavuni akijibu 'matusi' ya Kisiga katika lango lile lile la Kaskazini.

Matokeo hayo yalimaanisha kwamba timu ngeni katika ligi hiyo Ndanda FC inaendelea kubaki kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo baada ya mechi za mzunguko wa kwanza kufuatia ushindi wao mnono wa 4-1 dhidi ya wageni wenzao, Stand United ya Shinyanga.

Mabingwa Azam FC, ambayo juzi walishinda 3-1 dhidi ya Polisi Moro, wako katika nafasi ya pili.

Baada ya mechi ya jana, kocha wa Simba, Patrick Phiri alisema kuumia kwa Haruna Chanongo kuliwagharimu, kwa sababu kiungo huyo ndiye aliyekuwa akipeleka mashambulizi yote ya timu hiyo na pia safu yake ya ulinzi haiko vyema.

Phiri, ambaye timu yake ilimuacha katika dakika za lala-salama za kipindi cha usajili beki jembe wa msimu uliopita Mkenya Donald Musoti ili nafasi yake asajiliwe kiungo Mganda Okwi, alisema safu yake ya ulinzi ina mapungufu makubwa.

Kocha wa Coastal, Yusuph Chippo amesema kipindi cha kwanza chote alikuwa anawasoma Simba ndiyo maana akawaficha wachezaji wake kadhaa nyota akiwamo Mganda Yayo.

Aalisema anafahamu kwamba hakuna mtu aliyetegemea kama angewaacha nje wachezaji wazuri kama Yayo, lakini alifanya hivyo kwa makusudi na kwamba alitumia mbinu zaidi kuichezamechi hiyo.

Alisema alijua kwamba Simba ingeanza kwa kushambalia sana ndiyo maana akawaanzisha wachezaji wa kukaba zaidi.

Vikosi vilikuwa; Simba: Ivo Mapunda, Miraji Adam, Mohammed Hussein, Hassan Isihaka, Joseph Owino, Amissi Tambwe/ Raphael Kiongera (dk.64)/ Amri Kiemba (dk.89), Haroun Chanongo/ Uhuru Selemani (dk.35), Shabani Kisiga, Pierre Kwizera, Emmanuel Okwi na Ramadhan Singano 'Messi'.

Coastal: Shabani Kado, Hamad Juma, Sabri Rashid, Abdallah Mfuko, Hamis Kibacha, Tumba Lui, Selemani Rajab/ Lutimba Yayo (dk.47), Razack Khalfani/ Ayoub Yahaya (dk.47), Itubu Imbeb, Rama Salim na Joseph Mahundi.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA