BIN KLEB AANZA KUMFUNGIA KAZI OKWI

Baada ya Yanga 'kupigwa' na wapinzani wao wa jadi, Simba ambao wametangaza kumsajili kwa mara nyingine Mganda Emmanuel Okwi aliyeichezea msimu uliopita, hatimaye umeamua kumrejesha aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano, Abdallah Bin Kleb, kuwa mjumbe wa kamati hiyo.

Hata hivyo, mustakabali wa sakata la Okwi kukubaliwa kuichezea Simba au la linatarajiwa kutolewa ufafanuzi Septemba 6, mwaka huu wakati Kamati ya Mashindano na Haki za Wachezaji ya TFF itakapokutana.

Wakati Bin Kleb akiwa mwenyekiti wa kamati ya usajili ndiye aliyefanikisha usajili wa Okwi, huku akishinda vita ya kuwania pia saini ya Mbuyu Twite aliyekuwa amekula fedha za usajili za Simba kwa makubaliano ya kuichezea.


Bin Kleb pia ana historia nzuri Yanga kutokana na kufanikiwa kumrejesha Mrisho Ngasa akitokea Simba pamoja na kunasa saini za nyota kama Hamisi Kiiza, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu ambaye amemaliza mkataba na kujiunga na Azam.

Hata hivyo, zikiwa zimebaki siku chache kabla ya msimu mpya wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara haujaanza, uongozi wa klabu ya Yanga, jana umetangaza kamati tatu mpya huku ikimrejesha Bin Kleb kuwa mjumbe wa kamati hiyo.

Viongozi wa juu wa Yanga hivi karibuni walitangaza wajumbe wapya wa Kamati ya Utendaji na kuliacha 'pembeni' jina la Binkleb kwenye uongozi.

Akizungumza na gazeti hili jana mchana, Bin Kleb, alisema bado hajapata  taarifa za uteuzi huo ambao Yanga umeufanya jana na kwamba hana tatizo lolote na maamuzi hayo yaliyofanywa na viongozi wa klabu hiyo.

Wamejipanga: Yanga wako tayari kufa na Okwi katika usajili wake Simba msimu huu

"Sina taarifa rasmi, ila nimeambiwa na watu wawili kuhusiana na uteuzi huo," alisema Bin Kleb ambaye awali baada ya kuachwa alidai kwamba ndiye ambaye aliomba kupumzika katika nafasi aliyokuwa akiishikilia ya mwenyekiti wa kamati ya mashindano kutokana na kubanwa na majukumu yake binafsi.

Afisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema jana kuwa wajumbe wengine wa kamati ya mashindano ni pamoja na Cheyo Magembe, Ibrahim Didi, Hussein Ndama, Moses Katabalo, Mudhamiri Katunzi, Pascal Kihanga, Ray Kingo, David Luhago, Samwel Lukumay, Innocent Macha, Jackson Maige, Mugaya Mahende, Sule Makay, Michael Malebo na Paul Malume.

Wengine ni pamoja na Timothy Mbise, Mlangwa David, John Mogha, John Mutaboyerwa, Said Ntimizi, Lameck Nyambaya, Hussein Nyika, Fulgence Ramadhan, Ahmed Rashid, Majid Suleman, Frank Tenga na Beda Tindwa.    

Wajumbe wa Kamati ya Ufundi ni Nassoro Duduma, Roger Lamlembe, Pascal Malulu, Peter Msolla na Steve Zangira wakati wanaounda Kamati ya Soka la Vijana na Wanawake ni Shabani Katwila, Jessica Kabisa, Isack Mazwile, George Mwita na Ally Mayay Tembele.

Kizuguto alisema Wajumbe wenza wa Kamati ya Utendaji ya  klabu hiyo (Maendelo ya Michezo), Seif Ahmed na Isaac Chanji, ndiyo watakuwa wenyekiti wa kamati zilizotajwa hapo juu.

Aliongeza kuwa, Kamati ya Utendaji ya Yanga inawakaribisha wajumbe waliotajwa katika kamati hizo kwa dhamira njema kusaidia kuijenga klabu hiyo na wanaomba kupewa ushirikiano kutoka kwa Wana-Yanga wote ili waweze kutekeleza kazi zao vyema.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA