SIMBA KUSHUKA TENA DIMBANI LEO NA MAFUNZO

Wakati Simba ikitarajia kucheza mechi ya kirafiki leo dhidi ya timu ya Mafunzo ya Zanzibar, kocha Patrick Phiri amesema anatarajia kupata kikosi cha kwanza baada ya Raphael Kiongera kuungana na wachezaji wenzake.

Hii itakuwa ni mechi ya pili ya kirafiki kwa kikosi hicho cha Phiri, baada ya ile ya awali dhidi ya Kilimani City ambayo Simba iliibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Akizungumza jana kwa njia ya simu mara baada ya mazoezi ya timu hiyo, Phiri alisema Kiongera anatarajia kuwasili mwishoni mwa wiki, huku kikosi cha kwanza ambacho kitaanza kucheza katika michuano ya Ligi Kuu ya Bara kitajulikana wiki moja kabla ya michuano hiyo kuanza.


Phiri alisema kwa sasa ni vigumu kutangaza kikosi cha kwanza kwa vile wachezaji wengine waliosajiliwa na timu hiyo bado hawajawasili kuungana na wenzao katika mazoezi. Ligi Kuu ya Bara itaanza Septemba 20.

Mzambia huyo alisema kwa sasa pamoja na mazoezi ataendelea kusaka mechi na kirafiki dhidi ya timu zitakazoshiriki Ligi Kuu, kwani zitasaidia kumpa picha ya kile anachopaswa kukitarajia kwenye ligi.

Alisema baada ya mechi ya leo dhidi ya Mafunzo ya Zanzibar itakayopigwa kwenye Uwanja wa Amaan, wanatarajia kucheza dhidi ya Mtibwa Sugar Septemba 6, huku wakiendelea kusubiri mechi ya kirafiki ya kimataifa.

Alisema katika mechi yao ya awali dhidi ya Kilimani City, licha ya kwamba walishinda, hakuridhika na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake.

"Bado nahitaji kiwango zaidi katika timu yangu, lengo langu ni kufanya vizuri msimu huu katika ligi kuu ya Bara," alisema Phiri.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA