NI SAHIHI KWELI LOGARUSIC KUTUPIWA VIRAGO SIMBA!

Na Prince Hoza

Masaa yanayoyoma nilipeni changu kabisa niondoke: ndivyo ishara ya picha hii inavyojionyesha, Loga amefutwa kazi jana

HATIMAYE Klabu ya Simba imemtimua kazi Kocha Mkuu wao, Mcroatia Zdravko Logarusic kwa madai ya kukiuka taratibu na miiko ya klabu hiyo.

Hatua hiyo imefikiwa ikiwa ni siku moja baada ya Loga kuiongoza timu hiyo kupokea kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Zesco ya Zambia kwenye mechi ya Tamasha la Simba maarufu kama 'Simba Day' lililofanyika Uwanja wa Taifa Jumamosi.

Klabu ya Yanga, Desemba mwaka jana ilimtimua Kocha wake Mkuu, Mholanzi Ernie Brandts ikiwa ni siku mbili baada ya kufungwa 3-1 na watani zao, Simba katika mechi ya ndondo ya 'Nani Mtani Jembe' iliyoandaliwa na wadhamini wao wakuu Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia bia yake ya Kilimanjaro.

Ingawa Simba haikuwa tayari kueleza kwa kina miiko na taratibu alizokiuka kocha huyo, lakini habari za ndani kutoka chanzo chetu ndani ya klabu hiyo zinadai kuwa kiwango kibovu kilichoonyeshwa na kikosi chake dhidi ya Zesco kimechangia kutimuliwa kwake.


Akizungumza na waandishi wa habari jumapili katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, Rais wa Simba, Evance Aveva, alisema wameamua kusitisha mkataba na kocha huyo kutokana na kukiuka taratibu na miiko ya Simba.

Bila kufafanua zaidi alisema walishamuonya Loga siku nyingi lakini hakutaka kusikia na kwamba kuhusu taratibu za kuvunja mkataba ni siri ya uongozi na kocha huyo."Kuanzia sasa timu itakuwa chini ya kocha  msaidizi, Seleman Matola mpaka hapo atakapotangazwa kocha mwingine," alisema Aveva, huku akisisitiza kwamba kutimuliwa kwa kocha huyo hakutokani na matokeo ya mechi dhidi ya Zesco.

Mwezi uliopita Loga alipewa mkataba wa mwaka mmoja wa kuinoa Simba na alishaanza kuisuka upya timu hiyo kwa kuagiza idara ambazo aliziona zimepwaya msimu uliopita kusajiliwa wachezaji wapya.

Uongozi wa Simba kupitia rais wake Aveva umesema umeamua kumfuta kazi Loga kwa madai ya amekuwa mkali kwa wachezaji wake kitendo kinachodaiwa kufanywa na kocha huyo, Loga amekuwa na matatizo hayo kwa muda mrefu lakini alionywa.

Kabla ajaongeza mkataba mpya, Loga alikaa chini na uongozi wa Simba na kukubaliana masharti kisha baadaye akasaini mkataba wa mwaka mmoja, ina maana walishamalizana, uongozi wa Simba naona umeshindwa kuweka hadharani kuhusu maamuzi yao ya kumtimua.

Inajulikana wazi kuwa matokeo ya goli 3-0 iliyopata klabu yake ya Simba ndio sababu zilizopelekea kocha huyo kufutwa kazi licha ya rais Aveva kukataa kuweka wazi, Simba ilifungwa na Zesco ya Zambia mabao 3-0 katika uwanja wa Taifa Jumamosi iliyopita mchezo ukiwa wa kuadhimisha Simba Day.

Matokeo hayo yalimkera kila mtu hasa shabiki wa Simba ambao walishindwa kuamini huku wakipokea dhihaka kutoka kwa watani zao Yanga, Simba ilitimua tamasha hilo kuonyesha kikosi chake kipya kitachoshiriki ligi kuu msimu ujao.

Mungu wangu: kama anavyoonekana pichani, Loga akiwa amejishika kichwa mara baada ya kufukuzwa kazi jana

Tayari Simba ilishafanya usajili wake ambao wenyewe wanauona ni mzuri hivyo walitaka kushuhudia makali yao, lakini kipigo toka kwa Zesco tena cha aibu kiliwaudhi wengi wakiwemo viongozi wa timu hiyo ambao baadaye walitoa adhabu kali kwa kocha huyo ya kumfuta kazi.

Wapo wadau wa soka wanaoona Logarusic ameonewa kwa uamuzi huo, wanasema ni mapema mno tena kwa mechi moja kumfuta kazi, wanaibeza kauli ya rais wa Simba Aveva kua wamemfukuza Loga kwa makosa mengine.

Wadau hao wanadai kuwa kama alifukuzwa kwa makosa mengine mbona alipewa mkataba wa mwaka mmoja, hivyo matokeo ndio adhabu yake, lakini nionavyo mimi Simba imefanya haraka kumfukuza Loga isitoshe alitoa mapendekezo yake na bado hayajafanyiwa kazi.

Loga hakutaka wachezaji wa kuletewa ili wafanye majaribio yeye alitaka wachezaji wenye uwezo ili wasajiliwe moja kwa moja kama wafanyavyo Ulaya, lakini uongozi wa Simba ulishindwa kumsikiliza na kuamua kumletea wachezaji wa kufanya majaribio toka nchi za Gambia na Botswana kitendo ambacho Loga hakukipenda.

Malumbano mengine kati ya Loga na uongozi ni pale ulipoamua kumsajili mlinda lango mfupi ambaye ni Hussein Sharrif 'Cassilas', Loga alimkataa kipa huyo licha ya uongozi kusisitiza kuwa ni kipa bora msimu uliopita lazima acheze Simba.

Loga akiwa na kikosi cha Simba wakati anakinoa msimu uliopita, tayari amefukuzwa kazi

Ni kweli Loga amekuwa mkali kwa wachezaji kiasi kwamba wanakuwa na woga hasa kutokana na kauli zake zinazodaiwa ni matusi, msimu uliopita Loga hakuwa na maelewano mazuri na wachezaji wake Joseph Owino na Betram Mwombeki, Mwombeki kwa sasa ametemwa katika usajili wa kikosi hicho kwa madai ya kushuka kiwango.

Lakini mchezaji huyo alikuwa tegemeo katika kikosi cha Simba kiasi kwamba kumaliza ukame wa mastraika baada ya kuondoka Emmanuel Okwi, Mussa Hassan Mgosi na wengineo, Mwombeki alifanya vizuri katika kikosi cha Simba wakati kinanolewa na Abdallah Kibaden 'King'.

Kutimuliwa kwa Loga kunaongeza presha kwa kocha ajaye katika kikosi hicho, kitakwimu za haraka haraka Loga ameiongoza Simba kucheza mechi 21 na kushinda mechi nane, kushindwa nane na kutoka sare tano sawa na wastani wa kushindwa mechi moja na sare mechi mbili, tuonane juma lijalo

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA