HARUNA NIYONZIMA AISHANGAA YANGA

Kiungo wa kimataifa wa timu ya Yanga ya Tanzania Bara, Haruna Niyonzima, amesema kitendo cha timu yake kutoshiriki mashindano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kwenye ardhi ya kwao, Rwanda kimemuumiza sana.

Yanga iliondolewa kushiriki mashindano ya Kombe la Kagame baada ya kutaka kuleta kikosi cha pili chini ya kocha msaidizi, Mbrazil, Leonardo Neiva, hivyo nafasi yao kuchukuliwa na Azam.

Akizungumza kwa njia ya simu kutoka Dar es Salaam, Niyonzima, alisema alitamani sana kushiriki mashindano hayo na anaamini Yanga ingechukua kombe la michuano hiyo.


Niyonzima alisema hatua hiyo bado itaendelea kumsumbua akili yake, lakini anaheshimu maamuzi yaliyofanywa na viongozi wake.

"Imeniumiza sana, nilikuwa nimejiandaa sana kuitumikia timu yangu, lakini sisi Wanyarwanda huwa tunasema jikune pale mkono unapofika na usipofika omba msaada," alisema Niyonzima.

Nahodha huyo wa timu ya Taifa ya Rwanda (Amavubi), alisema pia atahakikisha anatoa mchango wake kwa Yanga katika kiwango cha juu ili waweze kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ambao waliupoteza msimu uliopita.

"Nilicheza Kagame Cup nyumbani mwaka 2010 nikiwa na APR na kuchukua ubingwa, mwaka huu nilijua ningeweka rekodi nyingine nikiwa na Yanga, lakini Mungu hakupanga, sijui kama naweza tena kupata nafasi hiyo kwa sababu maisha yanasonga mbele nami sijui nitakuwa wapi tena miaka inayokuja," alihitimisha.

Agosti 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Amahoro, kiungo huyo aliiongoza vyema Amavubi kuiondoa Congo Brazaville na kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON).

Alisema tayari alikuwa na mashabiki wengi ambao walijiandaa kuishangilia Yanga kwa sababu yake lakini mipango na ndoto hizo zimeyeyuka.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA