AZAM YAIFUMUA KMKM 4-0

AZAM FC jana walitoa ujumbe mzito kwa wapinzani wao katika Kombe la Kagame la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati wakati walipoifunga timu ya KMKM ya Zanzibar kwa magoli 4-0 katika mechi yao ya pili ya Kundi A kwenye Uwanja wa Amahoro hapa Rwanda.


Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Haiti, Leonel Saint Preux, aliifungia Azam magoli mawili ya kipindi cha kwanza baada ya nahodha John Bocco 'Adebayor' kuifungia timu hiyo goli la kuongoza katika dakika ya kwanza ya mchezo akimalizia kwa kichwa krosi ya Himid Mao.

Preux alifunga goli la pili la Azam na kwanza kwake jana katika dakika ya 18 akimalizia mpira uliotemwa na kipa wa KMKM, Mudathir Khamis na akafunga la tatu katika dakika ya 29 akimalizia pasi ya Mao tena.

Bocco tena akakamilisha kipigo hicho kizito kwa Wazanzibar kwa kufunga bao la nne katika dakika ya 52 akiunganisha krosi ya Shomari Kapombe. Bocco angeweza kufunga 'hat-trick' kama mpira wake mwingine wa mapema usingegonga nguzo ya lango wakati kipa Khamis akiwa ameshakubali 'matokeo'.

Ushindi umeifanya Azam ambayo iliingia kwenye michuano katika dakika za mwisho kuchukua nafasi ya Yanga iliyotaka kupeleka timu B, kufikisha pointi 4 baada ya mechi mbili.

Katika mechi ya awali dhidi ya wenyeji Rayon iliyomalizika kwa sare ya 0-0, Azam pia walitawala mchezo na wengeweza kuibuka na ushindi kama wasingepoteza nafasi nyingi za kufunga ikiwamo shuti la Kipre Tchetche lililogonga 'besela', huku pia Salum Aboubakar 'Sure Boy' akishindwa kufunga katika nafasi ya wazi jirani na lango kwa kupiga 'funika' na kutoa nje mpira ambao angeweza kufunga kirahisi kama angepigia kwa pembeni ya kiatu.

Mabingwa Vital'O wanatarajia kushuka dimbani tena leo kucheza dhidi ya wenyeji Polisi ya Rwanda, wakati Benadir ya Somalia itaikabili El Mereikh ya Sudan na Gor Mahia ya Kenya watawavaa Atletico ya Burundi.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA