TAIFA STARS HAIKAMATIKI........

Timu ya soka ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ilitinga hatua ya pili ya mchujo ya kuwania kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika 2015 kufuatia sare ya 2-2 ugenini iliyowapa ushindi wa jumla wa 3-2 dhidi ya Zimbabwe kwenye Uwanja wa Taifa jijini Harare jana.

Matokeo hayo yanamaanisha kwamba Stars sasa itaikabili Msumbiji ambayo iliing'oa Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 5-0 katika mechi ya hatua ya pili ya mchujo itakayofanyika nyumbani wikiendi ya Julai 18-20 na ya marudiano ugenini Maputo wikiendi ya Agosti 1-3. Mshindi baina ya Stars na Msumbuji ataingia katika hatua ya makundi.


Endapo Tanzania itaitoa Msumbiji itaingia katika Kundi F la kufuzu ambalo linaundwa na timu za Zambia, Niger, Cape Verde.

Timu mbili kutoka kila kundi la kuwania kufuzu kati ya makundi saba yaliyopo, pamoja na mshindi wa tatu mmoja aliyefanya vizuri zaidi, wataungana na wenyeji Morocco kwa ajili ya fainali hizo za Mataifa ya Afrika 2015 nchini Morocco.

Stars jana ilianza vibaya mechi baada ya kujikuta ikitanguliwa kwa goli la mapema katika dakika ya 13 lililofungwa na Danny Phiri.

Hata hivyo, Stars ilicharuka na kusawazisha goli hilo dakika 13 baadaye lililofungwa na beki wa kati Nadir Haroub 'Cannavaro'.

Stars, ambayo katika mechi ya awali jijini Dar es Salaam iliifunga The Mighty Warriors 1-0 kwa bao la mshambuliaji wa Azam FC, John Bocco 'Adebayor', ilijiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kusonga mbele katika michuano hiyo ya Afrika wakati mshambuliaji wa TP Mazembe, Thomas Ulimwengu alipoifungia goli la kuongoza katika dakika ya 46.

Hata hivyo, Zimbabwe walihitaji dakika tisa tu kusawazisha bao hilo kupitia kwa Katsande na kufanya dakika za mwisho za mechi hiyo kuwa ngumu kwa wageni wakati wenyeji wakisaka magoli mawili waliyohitaji ili kusonga mbele.

Stars inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager ilikwenda Msumbiji chini ya mkuu wa msafara Rais wa Shirikisho la Soka (TFF), Jamal Malinzi na ilipokewa na hisia za 'mizengwe' baada ya kudaiwa kunyimwa funguo za vyumba katika hoteli waliyofikia, kwa mujibu wa ripoti za kutoka nchini humo.

Kwa mujibu wa takwimu za mechi ya jana, Zimbabwe ilikaa na mpira kwa asilimia 52 dhidi ya asilimia 48 za Stars, Zimbabwe ilipia kona 5 dhidi ya 2 za Stars, huku pia wenyeji wakifanya majaribio ya kufunga 6 dhidi ya manne ya Stars.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA