NEYMAR AANZA KUUTAFUTA UFALME BRAZIL AIONGOZA KUIA CROATIA 3-1

MWANZO mzuri kwa Neymar akifunga mabao mawili usiku wa jana, wenyeji Brazil wakianza vyema Fainali za Kombe la Dunia kwa ushindi wa 3-1 dhidi ya Croatia Uwanja wa Corinthias, mjini Sao Paulo.


Croatia waliotawala sehemu ya kiungo, waliuanza vizuri mchezo na kufanikiwa kupata bao la kuongoza dakika ya 11.
Sifa zimuendee Olic aliyepiga krosi nzuri kwa Nikica Jelavic na katika harakati za kuokoa, Marcelo wa Brazil aliutumbukiza mpira kwenye lango lake.

Neymar akimfunga kwa penalti kipa Stipe Pletikosa wa Croatia aliyekaribia kuokoa mkwaju huo kama si kuupangulia nyavuni kwake

Croatia waliendelea kutawala mchezo baada ya bao hilo, lakini Brazil waiendelea nao kupambana kusaka bao la kusawazisha.

Juhudi hizo zilizaa matunda dakika ya 29 baada ya Neymar kuisawazishia Brazil kufuatia shambulizi la kushitukiza- baada ya kipa Julio Cesar kuokoa mpira wa kichwa wa Jelavic na kuanzisha shambulizi haraka.

Brazil ilipata bao la ushindi kwa penalti dakika ya 71 baada ya Fred kujiangusha wakati anakabiliana na Dejan Lovren kwenye eneo la hatari na Neymar akaenda kufunga tena.

Oscar alihitimisha ushindi wa Brazil kwa bao la tatu dakika ya 90 na ushei na kuwapa faraja mashabiki wa nyumbani.

Kikosi cha Brazil kilikuwa: Julio Cesar, Dani Alves, Thiago Silva, Luiz, Marcelo, Paulinho/Hernanes dk63, Gustavo, Hulk/Bernard dk68, Oscar, Neymar/Ramires dk88 na Fred.

Croatia: Pletikosa, Srna, Corluka, Lovren, Vrsaljko, Modric, Rakitic, Perisic, Kovacic/Brozovic dk61, Olic na Jelavic/Rebic dk78.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA