MALINZI AIKATAKATA YANGA, APINGA MANJI KUONGEZEWA MWAKA MMOJA
Wanachama wa Yanga waliokutana Juni Mosi, mwaka huu katika mkutano wa marekebisho ya katiba, pia walikubaliana kusogeza mbele uchaguzi mkuu wa klabu hiyo hadi Juni 15, mwakani.
Hata hivyo, baadhi ya wanachama wa Yanga wakiongozwa na Juma Magoma mwenye kadi namba 2319, wamepinga maamuzi hayo na kumuandikia Malinzi barua ya kutaka asaidie klabu yao ifanye uchaguzi ndani ya siku 90 na ili katiba yao isivunjwe.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka nchini Brazil jana mchana, Malinzi, alisema bado hajaiona barua hiyo ya wanachama wa Yanga iliyondikwa tangu Juni 5, mwaka huu na kupelekwa katika ofisi ya kiongozi huyo.
Malinzi alisema licha ya kutoipata barua hiyo kutokana na yeye kuwa nje ya nchi, uongozi wake muda wote utahakikisha wanachama wake wanafuata taratibu, kanuni na katiba zao.
"Kuhusiana na barua ya wanachama wa Yanga siwezi kusema chochote, niko kwenye mikutano ya CAF/Fifa, sijaiona barua hiyo," alisema kwa kifupi Malinzi.
Wanachama hao katika barua yao walisema kuwa kuruhusu viongozi waliopo kuendelea kuwaongoza kwa kipindi cha mwaka mmoja ni kudhihirisha wazi wote hawaifahamu Katiba ya Yanga, TFF na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Alisema kwa mujibu wa Katiba ya Yanga uongozi unapomaliza muda wake madarakani na kulazimika kuongezewa, wanatakiwa kuongezwa muda wa siku 90 na baada ya hapo kuitishwa uchaguzi mkuu na si vinginevyo.
Naye Goefrey Mwaipopo (2481), alisema wanashangaa kuona Mama Fatma Karume anaitwa mdhamini wakati jina lake haliko kwenye orodha ya wadhamini wa klabu hiyo.
Viongozi wa Yanga ambao wanamaliza muda wao kikatiba wa miaka minne waliingia madarakani katika uchaguzi uliofanyika mwaka 2010, hivyo kwa kauli hiyo ya Malinzi kama ataitekeleza ni wazi Yanga watalazimika kufanya uchaguzi baada ya siku 90 na si mwakani kama walivyopitisha katika mkutano mkuu.