MAKALA: ACHENI PROPAGANDA, WAMBURA SIYO YANGA
(Mbabe: Wambura akiwapungia wafuasi wake mara baada ya kutangazwa mshindi wa rufaa yake aliyopinga kuenguliwa Simba.
MARA baada ya kamati ya rufaa ya shirikisho la soka nchini TFF kutengua maamuzi ya kamati ya uchaguzi ya klabu ya Simba inayoongozwa na mwanasheria Damas Daniel Ndumbaro na kumrudisha tena katika kinyang'anyiro cha uchaguzi wa klabu hiyo Michael Richard Wambura.
Awali kamati ya uchaguzi ya klabu ya Simba ilimuengua Wambura kwa madai hana sifa ya kuwa mgombea, Wambura ilidaiwa alisimamishwa uanachama tangia mwaka 2010 baada ya kuupeleka mahakamani uongozi wa Simba.
Kipindi hicho Simba ilikuwa chini yake Hassan Dalali 'Field Marshall', Wambura alisimamishwa uanachama baada ya kuvunja katiba ya Simba, TFF, CAF na FIFA.
Kutokana na maamuzi hayo ya kamati ya Ndumbaro, Wambura alikata rufaa TFF kupinga kuenguliwa kwake, mwanzoni mwa wiki hii kamati ya rufaa ya TFF inayoongozwa na mwanasheria Julius Lugaziya ilipitia rufaa hiyo na kujiridhisha kuwa Wambura alionewa hivyo ilimrudisha katika kinyang'anyiro hicho, Lugaziya alisema Wambura ni mwanachama halali tofauti na mapingamizi matano yaliyoletwa kwake na wanachamawa Simba ambao walimpinga Wambura.
Lugaziya aliendelea kusema kuwa katiba ya Simba inakataza kupeleka masuala ya soka mahakamani hivyo Wambura ni batili, lakini akashangaa kuwa Wambura ni batili mbona hakukuwepo na zuio lolote kwa mwanachama huyo kushiriki vikao vya maamuzi.
(Mwenyekiti wa kundi la marafiki wa Simba F.O.S linalodaiwa kumpinga Wambura)
Wambura ameshiriki vikao vyote vinne vya mkutano wa kawaida na kushiriki mikutano miwili ya maamuzi ikiwemo ya marekebisho ya katiba na kuteua kamati ya uchaguzi ambayo ndiyo iliyomuengua.
Kwa maana hiyo katiba ya Simba na kamati ya uchaguzi zote ni batili kama tutakubaliana kuwa Wambura ni batili, hivyo ni busara kumrudisha, na wajumbe watano wa kamati hiyo walipiga kura ya kumrejesha ama kumuengua.
Kura tatu zilitosha kumrejesha Wambura katika uchaguzi huo wakati kura mbili zilimkataa, hivyo Lugaziya alitangaza kumrejesha Wambura katika nafasi yake ya kuwania urais katika klabu ya Simba.
Akitangaza hayo kundi la wanachama wa klabu hiyo yenye makazi yake mtaa Msimbazi, Kariakoo wilayani Ilala mkioani Dar es Salaam walikuja juu na kuendelea kumpinga vikali Wambura, huku wakiishutumu TFF kwa kumbeba mgombea huyo wa urais.
(pichani mwenyekiti wa kamati ya rufaa ya TFF Julius Lugaziya akitangaza maamuzi ya kamati yake iliyomrudisha Wambura katika kinyang'anyiro cha uhaguzi wa Simba SC)
Mbali zaidi wanachama hao wakiungwa mkono na kundi la marafiki wa Simba walidai Wambura ni Yanga hivyo haitawezekana mtu wa Yanga aiongoze Simba.Nianavyo mimi wanachama wa Simba watulie na wasubiri siku ya uchaguzi ili wafanye maamuzi sahihi, Wambura siyo Yanga ni Simba kama walivyo wengine isipokuwa ile ni misimamo yake tu, siku zote watu hupingana hata baba moja mama moja.
Tukijiridhisha Wambura ni Yanga basi hatutaweza kumjua Simba halisi, Wana-Simba wote wenye mapenzi na timu yao hupigania kila kimoja wapo cha Simba ili mradi mali yao isipotee, Wambura amekuwa jasili mno na kuwaandama wale wote wanaokwenda kinyume.
Ni haki yake kama mwana-Simba kwani mtu wa Yanga hawezi kuhoji mali za Simba, nimemsikia sana Wambura akilalamikia utafunwaji na ubadhilifu wa mali za Simba.
Kumtuhumu kuwa yeye ni Yanga ni propaganda chafu zenye lengo la kumharibia asipate anachokitaka na vile vile kuharibu sifa yake kama mwana-Simba na kumtengenezea chuki kwa wale wanaomuamini, si vizuri kwa mtu kumchafua mwenzake hasa kwa kuhamisha hisia zake za kiitikadi.
Wambura ni Simba kama wengine na si Yanga, kama kuna mtu anao ushahidi kuwa Wambura ni Yanga basi anaweza kuutoa na si kuzungumza hovyo kwenye vyombo vya habari.
Mwisho, kama Wambura ni Yanga basi kamati ya Ndumbaro ni Yanga kwani alishiriki kuiteua, katiba ya klabu ya Simba nayo ni Yanga kwani alishiriki kuitengeneza kwakuwa ni mwanachama wa Simba na mwenye kadi.