TAIFA STARS YAINGIA KAMBINI, MAGODORO YAMCHELWESHA NGASA

Kikosi cha timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars) kilienda Mbeya jana kikitokea Dar es Salaam kwa ajili ya kuendelea na mazoezi ya kujiandaa na mechi ya marudiano dhidi ya Zimbabwe bila ya nyota wake watatu akiwamo mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngasa.


Wachezaji wengine ambao hawakuondoka jijini jana kuelekea Mbeya kwenye kambi hiyo ni pamoja na Ramadhan Singano 'Messi' wa Simba na kipa Deogratius Munishi 'Dida' kutoka Yanga.

Akizungumza jana, Ngasa alisema ni kweli hawajaondoka ila wana ruhusa maalum.

Ngasa alisema kwamba wanatarajia kuondoka leo kuelekea Mbeya kuungana na wachezaji wenzao.

"Ni kweli hatujaondoka, lakini tuna ruhusa maalumu," alisema kwa kifupi mshambuliaji huyo.

Gazeti hili lilibaini kwamba nyota hao wa Taifa Stars, mshambuliaji wa timu ya taifa ya wanawake (Twiga Stars), Mwanahamisi Omary 'Gaucho' ni baadhi ya nyota waliokuwa wanashiriki kuandaa tangazo la biashara la magodoro.

Tangazo hilo lilikuwa linatengenezwa jana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Stars iliyo chini ya kocha mpya, Mholanzi Mart Nooij, itaenda ugenini Harare kusaka japo sare katika mechi yao ya marudiano itakayochezwa katika wikiendi ya kati ya Mei 30-31 na Juni 1. Ikivuka hatua hiyo itaingia raundi ya pili ya mchujo ambako itakutana na mshindi baina ya Sudan Kusini na Msumbiji.

Mshindi baina yao atatinga katika hatua ya makundi ya kuwania kufuzu. Endapo Tanzania itatinga hatua ya makundi ya kuwania kufuzu itajumuika katika Kundi F la kufuzu ambalo linaundwa na timu za Zambia, Niger, Cape Verde.

Timu mbili kutoka kila kundi la kuwania kufuzu kati ya makundi saba yaliyopo, pamoja na mshindi wa tatu mmoja aliyefanya vizuri zaidi, wataungana na wenyeji Morocco kwa ajili ya fainali hizo za Mataifa ya Afrika 2015 nchini Morocco.

Mara ya mwisho Taifa Stars kushiriki fainali hizo za AFCON ilikuwa ni mwaka 1980 wakati 2009 ilifanikiwa kucheza fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) zilizofanyika Ivory Coast ikiwa chini ya kocha wa wakati huo Mbrazil Marcio Maximo.

Katika kuhakikisha Stars inafanya vizuri katika mchezo huo wa marudiano, imeandaa usafiri wa basi wa kuelekea Harare kwa mashabiki wanaotaka kuishangilia timu hiyo kwa gharama ya Sh. 300,000 kwa kila mmoja.

John Bocco ndiye aliyeifungia Stars bao pekee lilioamua mechi ya kwanza dhidi ya Zimbabwe iliyochezwa Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA