MASIKINI! YANGA KUVUNJA MKATABA NA OKWI

Katika kile kinachoonekana Yanga imepanga kuachana na mshambuliaji wake Emmanuel Okwi, uongozi wa klabu hiyo umempa masharti magumu nyota huyo wa Uganda ili aendelee kukitumikia kikosi chao.

Akizungumza na waandishi kwenye ofisi za makao makuu ya Yanga jijini Dar es Salaam jana, makamu mwenyekiti wa klabu hiyo, Clement Sanga alisema wameamua kufanya mazungumzo na Okwi ili kumaliza tofauti zilizojitokeza kati ya uongozi wao na mkali huyo wa kufumania nyavu.

Uongozi wa Yanga jana ulikuwa umekutana kwa mazungumzo na wenyeviti na makatibu wakuu wa matawi ya klabu hiyo klabu hapo.

"Tuliingia mkataba na Okwi wa miaka miwili na nusu kwa sharti kwamba kibali chake cha kucheza mpira nchini atalipa mwenyewe.


Tulikubaliana naye atakuwa mchezaji wa Yanga lakini jukumu la kulipia kibali chake ni lake mwenyewe. Lakini nyote mnajua kwamba hajacheza mechi sita kwa sababu ya kuzuiwa na TFF (Shirikisho la Soka Tanzania), lile lilikuwa suala lake na TFF na si Yanga," alisema.

"Tumezungumza na Okwi kwa sababu hiki kipindi chake cha miaka miwili na nusu Yanga itabidi tubadilishe kwa sababu tumemkosa katika baadhi ya mechi. Tumemuomba aje tuupunguze mkataba wake na arudishe fedha au aje tuongeze muda uliopotea katika mkataba wake.

"Robo ya mkataba, asilimia 10 au 20 ya mkataba wake imepotea wakati akiwa kwenye harakati ya kupata kibali. Haya ndiyo mazugumzo yetu na yeye na kesho (leo) Katibu Mkuu (Beno Njovu) atamwandikia barua ya kumkumbusha," alisema zaidi kiongozi huyo.

Alisema Yanga haina haraka na straika huyo kwa sababu iliamua kumnasa ili aisaidie katika michuano ya kimataifa na si vinginevyo.

"Sisi hatuna haraka sana Okwi kwa sababu hatujamsajili kwa ajili ya mashindano ya hapa ndani bali michuano ya kimataifa. Kwa hiyo, bado tunao muda wa kujadiliana naye," alisema Sanga.

Okwi, mchezaji wa zamani wa Simba na SC Villa ya kwao Uganda, alijiunga na Yanga siku ya mwisho ya usajili wa dirisha dogo msimu huu Desemba 15 mwaka jana baada ya kuikacha klabu ya Etoile du Sahel (ESS) ya Tunisia lakini alikosa mechi kadhaa za Yanga za mzunguko wa pili baada ya kuzuiwa na TFF.

Mshambuliaji huyo tegemeo katika kikosi cha timu ya taifa ya Uganda (Cranes), aligoma kuichezea Yanga katika mechi za mwisho za mzunguko wa pili akitaka alipwe fedha zake za kusaini mkataba.

PLUIJM HAJALIPWA
Kuhusu kocha Mholanzi Hans van der Pluijm, uongozi wa Yanga ulisema jana kuwa ulitambua kwamba kocha huyo alikuja Tanzania kwa muda mfupi na hawatamnyima haki zake.

"Kulikuwa na siri kubwa juu ya kocha huyu lakini tulitambua kwamba anaondoka, wengi wakati tunamleta walisema kocha mzee, lakini sasa anaondoka wanauliza kwa nini anaondoka

Hatuwezi kumdhulumu pesa zake maana ana mapenzi makubwa na Yanga hadi ameomba uanchama na Jumapili atarudi hapa tumkabidhi pesa zake na yeye ndiye anayetusaidia kusajili na kupata mwalimu mzuri atakayekinoa kikosi chetu.

"Lakini si lazima tuwe na kocha wa kigeni tu, maana hata Watanzania pia wana uwezo. Mbeya City iko chini ya kocha mzawa lakini imefanya vizuri na tunapaswa kuwapongeza hilo. Kwa misingi hiyo hata sisi viongozi bado tunayo nafasi ya kuamua kocha tumtakaye," alisema zaidi Sanga.

DOMAYO, KAVUMBAGU
Kuhusu kuondoka kwa wachezaji wao wawili Didier Kavumbagu na Frank Domayo, uongozi wa Yanga umesema siyo mwisho wa  Yanga, kwani unaendelea na mipango ya kuhakikisha unasajli wachezaji wengine wazuri ambao wataisadia timu kwenye msimu ujao.

Sanga alisema kuondoka kwa Kavumbagu ni kutokana na kuchelewa kwa majibu ya TFF juu ya idadi ya wachezaji wageni kwa msimu mpya, huku Domayo ambaye tangu mwaka jana aliombwa kuongeza mkataba alikuwa akisema anamsubiri mjomba wake ndipo aweze kufanya hivyo.

TANDALE MARUFUKU YANGA
Aidha, uongozi wa Yanga umelifuta rasmi tawi la Tandale kwa madai kuwa limekuwa chanzo cha vurugu na migogoro ndani ya klabu.

Pia uongozi wa klabu hiyo umewafuta uanachama wanachama sita ambao walikiuka katiba ya Yanga kwa kwenda kuongea na waandishi na habari bila ya idhini ya uongozi huku pia wakishindwa kulipia ada zao za uanachama kwa zaidi ya miezi sita.

Waliofutwa uanachama ni Ally Kamtande, Isiaka Dude, Hamisi Matandula, Waziri Jitu Ramadhani, Mohamed Kigali Ndimba na Seleman Hassan Migali.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga umesema mkutano mkuu wa mabadiliko ya katiba utafanyika Juni Mosi mwaka huu kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi uliopo Oysterbay jijini Dar es Salaam huku ukiwataka wanachama wote kulipa ada za uanachama ili wahuhudhirie mkutano huo wakiwa hai.

kuhusu ujenzi wa uwanja mpya wa kisasa kwenye eneo la Jangwani, uongozi umesema bado unaendelea na mpango huo na kinachosubiriwa ni majibu ya serikali juu ya maombi ya eneo la ziada, kwa vile Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam amesema suala hilo lipo ukingoni.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA