MAKALA; KAMATI YA UCHAGUZI SIMBA KUMBE BOMU.

Na Prince Hoza

KAMATI ya uchaguzi ya klabu ya Simba inayoongozwa na mwanasheria Dk Damas Daniel Ndumbaro imeonyesha kasoro nyingi na kukosa weledi baada ya kumtupa nje aliyekuwa mgombea nafasi ya urais katika klabu ya Simba Michael Richard Wambura.

Wambura ameondolewa katika kinyang'anyiro hicho kwa madai si mwanachama halali wa Simba pia aliwahi kusimamishwa uanachama wake tangia mwaka 2010 wakati huo mwenyekiti akiwa Hassan Dalali 'Field Marshal'.


Ndumbaro alitangaza rasmi kumuondoa katika kinyang'anyiro hicho baada ya kamati kuridhika na maelezo ya waweka pingamizi, akitangaza maamuzi hayo Ndumbaro alisema Wambura aliwahi kuishitaki klabu ya Simba mahakamani hivyo ametenda kosa kubwa la kuikiuka katiba ya Simba, TFF na Fifa ambapo inakataza masuala ya soka kupelekwa mahakama za kiraia.

Hivyo alisimamishwa uanachama wake na uongozi wa Simba pia jina lake lilienguliwa katika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo uliofanyika mwaka 2010 uliomuweka madarakani Alhaj Ismail Aden Rage.

Kwanini kamati hiyo inayoongozwa na mtu makini na mwanasheria nadiriki kuiita bomu! Ndumbaro ameonyesha jinsi gani alivyoshindwa kutumia uanasheria wake na kuiongoza kiweledi kamati hiyo nyeti na nzito kwa klabu ya Simba.

Ndumbaro amekurupuka na kutoa maamuzi ya kishabiki na yenye kuleta mvurugano mkubwa ndani ya Simba, hakuna hata pingamizi moja lenye mashiko linaloweza kumbana Wambura.

Wakati akiwania uongozi ndani ya TFF yeye na Jamal Malinzi walienguliwa na kamati ya uchaguzi ya TFF iliyokuwa chini yake Himid Mbwezeleni kwa makosa mbalimbali.

Hata hivyo sakata la uchaguzi huo lilifika Fifa na baadaye Fifa iliagiza mchakato wa uchaguzi huo uanze upya na wote wakaruhusiwa kugombea, ina maana waliondolewa makosa yao.

Hapo dnipo Malinzi alipopata nafasi ya kuwania urais na kuibuka kidedea, Malinzi alipoingia madarakani alitangaza kufuta na kusamehe adhabu zote za vifungo kwa wanamichezo waliofungiwa maisha na TFF, vyama vya mikoa na vilabu.

Adhabu zote zilifutwa na ndio maana mwenyekiti wa klabu ya Simba akatumia nafasi hiyo kumteua Wambura kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji.

Wambura yuko huru kugombea na ndio maana alishiriki katika kuitengeneza katiba mpya ya Simba pamoja na kuteua kamati ya uchaguzi inayoongozwa na Ndumbaro, pia ni vema kuheshimu uteuzi wake kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji ya Simba uliofanywa na mwenyekiti halali wa klabu hiyo Ismail Aden Rage.

Ndumbaro aache ushabiki kama kazi imemshinda! nilimuheshimu sana kwa weledi wake lakini hafai na mchochezi, kwanza amekubali mapingamizi yakipuuzi ambayo yote yanaonekana kupandikizwa, pia yana uzandiki ndani yake.

Ili uchaguzi wa Simba ufanyike kwa amani basi wagombea wote waende kuomba kura kwa wanachama, narudia Wambura ni mwanachama halali kwani adhabu zote zilishafutwa na rais wa TFF Jamal Malinzi pamoja na Fifa, na kama asingekuwa mwanachama halali asingeteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji, Alamsiki

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA