REAL MADRID YAILAZA BAYERN MUNICH 1-0
Japo ni kwa ushindi finyu wa bao
1 bila - Real Madrid wamejiwekea akiba nzuri kibindoni na ndiyo
watakayoendeleza nayo kampeni yake ya kuwania kuipokonywa ubingwa wa
Champions league Bayern.
Karim Benzema ndie alitingisha wavu wa Bayern mapema katika kipindi cha kwanza.Mashambulio ya Christino Ronaldo yalikuwa yakisisimua lakini hayakuzaa matunda zaidi kwa Real. Juhudi za Bayern za kukomboa bao hilo zilizimwa kabisa - hivyo kuiwezesha Real kuendeleza rekodi yao ya kutoshindwa nyumbani kufikia mechi 18 .
Bayern sasa itajitahidi itumie vilivyo morali wa mashabiki wao nyumbani hapo jumanne kuwageuzia kibao Real. Mshindi atakutana na Chelsea AU Atletico Madrid, ikitegemea matokeo ya mechi yao ya Jumatano katika raundi yao ya pili ya nusu fainali hiyo.
Na kocha Jose Mourinho yu matatani tena... Ni miongoni mwa wafanyikazi watatu wa-Chelsea waliofunguliwa mashtaka na FA kwa madai ya kuonesha ukosefu wa nidhamu wakati wa mechi iliyowafedhehesha pale walipofungwa na Sunderland 2-1 , timu ambayo iko mkiani mwa league ya Premier.
Baada ya mechi hiyo Mourinho alitoa 'pongezi' tele hasa kwa refa Mike Dean na kumtaja kuwa mtu wa kustaajabisha sana kwa jinsi alvyoendesha mechi hiyo...na pia akampongeza mkuu wa bodi ya marefa Mike Riley- Sasa matamshi hayo yamechukuliwa kama kejeli za kuwashusha hadhi aliyowataja.
Amepewa mpaka 28 April kujibu mashtaka hayo. Wenzake mchezaji Ramires anasemekana alitishia kutumia nguvu uwanjani hasa pale alipobishana kwa sababu ya penalty iliyopewa Sunderland huku meneja msaidizi Faria pia anadaiwa alitumia lugha isiyostahili.
Si mara ya kwanza kocha Morihno anajikuta matatani kwa sababu ya tabia yake ya kutupa vijembe vya maneno kwa mahasimu wake lakini wengi wa wafuasi wake huvutiwa sana na mafumbo yake.
Tumalizie kwa mashindano ya klabu bora cha Voliboli ya wanawake wa Afrika yanayoendelea huko Tunisa.
Timu za Kenya zimekuwa zikifanya vizuri sana- Mojaapo ni bigwa watetezi magereza, imezishinda timu walizokuwa nao katika kundi moja za Aljeria , Cameroon na Misri na pia kushinda mechi yao ya jana ya robo fainali kwa seti tatu kwa bila dhidi ya timu kutoka Tunisia.Timu hiyo ya magereza wamelishinda kombe hilo mara 5 , kwa miaka minne ikiwa mfululizo.