MAKALA: TFF BORA LIENDE, UTEUZI WA AJABU TIMU YA TAIFA

Na Prince Hoza

MWISHONI mwa wiki iliyopita Tanzania iliadhimisha miaka 50 ya muungano wake uliotokana na mataifa mawili Tanganyika na Zanzibar ambapo waliunda taifa moja ambalo ni Tanzania.

Muungano huo umeweza kudumu kwa miaka 50 ambapo waasisi wa mataifa hayo mawili yaliyoungana nikiwazungumzia baba wa Taifa hayati Mwl Nyerere na hayati Abeid Amaan Karume, wote hao kwa sasa wametangulia mbele ya haki lakini tutawakumbuka sana kwa kutuletea muungano huo.

Licha ya muungano huo uliotimiza miaka 50 kutizamwa kwa jicho baya na baadhi ya Watanzania wachache ambao wamekuwa wakiujadili mara kwa mara, kuna wengine wakitaka uvunjwe huku pande nyingine zikitaka muungano wa mkataba.


Lakini yote kwa yote muungano umetimiza miaka 50 ambapo ulisherehekewa kwa vifijo na nderemo katika uwanja wa Uhuru na baadaye uwanja wa Taifa ambapo kulikuwa na pambano la soka kati ya timu ya taifa, Taifa Stars na timu ya taifa ya Burundi Itamba mulugamba.

Katika mchezo huo Burundi walifanikiwa kutibua sherehe za muungano baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0, magoli ya Didier Kavumbagu anayekipiga Yanga, Amissi Tambwe anayekipiga Simba na Ndikumana Sebbo yaliweza kutibua furaha ya Watanzania katika kusherehekea muungano wa miaka 50.

Kikosi cha Stars ndio kile kilichoteuliwa kwa mbwembwe zote na shirikisho la kandanda nchini TFF chini yake rais Jamal Malinzi, TFF iliteua wachezaji zaidi ya 60 ambao walitokana na jopo la makocha 20 waliotawanywa mikoa mbalimbali ya nchi.

Lengo likiwa ni kutengeneza timu ya taifa imara itakayofuzu fainali zijazo za mataifa Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Morocco, rais wa TFF aliahidi kurejesha msisimko wa mchezo wa soka nchini kwa kuteua nyota hao.

Mawazo ya Watanzania wengine waliamini kupatikana kwa kikosi hicho ndio mwisho wa Tanzania kuwa kichwa cha mwendawazimu, lakini baadhi yetu tulipinga uteuzi huo.

Mapema kabisa niliandika makala kupinga waziwazi uteuzi wa kikosi cha timu ya taifa kinachotokana na wachezaji wa kuokotezwa na kuwekwa kambini Tukuyu mkoani Mbeya, niliweka misimamo yangu na kuwaambia timu ya taifa imara inatokana na ligi imara.

Nilimwomba Malinzi ajaribu kuongeza timu ligi kuu badala ya 14 za sasa ambazo hazileti ushindani wowote kwa wachezaji, nilimuomba aongeze timu ili ziwe 18 au 20.

Nilitaka wadhamini wa ligi hiyo Vodacom wakubaliane na wazo hilo ili kuongeza ushindani na hatimaye ipatikane timu bora ya taifa, lakini wazo langu lilitupiliwa mbali kwa sababu mimi ngozi yangu nyeusi.

Ningekuwa mweupe kama Mourinho huenda ningefikiriwa, ukweli ndio huo wanamichezo wenzangu hasa mnaopenda soka, hatuwezi kuendelea na kupiga hatua kwa timu ile ya kuokoteza mchangani ambayo imewezwa kupigwa bakora 3-0 na Warundi.

Warundi bado kabisa kwa Tanzania, hawana uwezo wa kutufunga lakini kwakuwa Stars yetu ya uchochoroni ndio maana imepigwa magoli yale siku ile, Sijawahi kuona wala kusikia timu ya taifa ya nchi husika inachaguliwa kwa kuhusisha wachezaji wa mitaani.

Siku zote timu ya taifa inatokana na wachezaji wa ligi kuu, tena wale wanaotokea timu zilizofanya vizuri ama zile zilizoshika nafasi za juu, Kwa mfano wachezaji wengi wangetokea vilabu vya Azam fc, Yanga, Mbeya City na Simba.

Lakini timu yetu ya taifa imetoa wachezaji wengi kutoka Tukuyu sehemu ambayo naikumbuka kutokana na timu yake iliyowahi kupanda daraja na baadaye kuwamabingwa wa bara, lakini kule walikwenda kuweka kambi tu ya muda.

Hazijapita siku mbili tangia Stars itoke kupokea kipigo kutoka kwa Warundi, kocha mpya wa timu ya taifa, Taifa Stars Mholanzi Mart Nooij alitangaza wachezaji wengine tisa kuunda kuongeza nguvu kikosi hicho.

Hiyo ni aibu ya kuzomewa na mashabiki kufuatia kipigo ilichopata toka kwa Burundi, mashabiki wa soka waliiizomea Stars kufuatia kipigo hicho huku wakisikika kukipinga kwa nguvu zote kikosi hicho cha mchangani.

Bado ndani ya shirikisho la kandanda nchini TFF kuna viongozi wasiojua mpira, wamechaguliwa kutokana na elimu zao lakini masuala ya soka wajuaji wametoweka kwakuwa hawana elimu.

Kati ya wachezaji tisa walioteuliwa mmoja ana mapungufu, Shomari Kapombe amekuwepo nchini kwa muda mrefu pasipo kucheza soka la ushindani, Kapombe anadaiwa kuisusa klabu yake ya AS Cannes ya Ufaransa ambapo alisajiliwa kwa mkataba wa miaka miwili.

Lakini jina lake nimeliona katika uteuzi wa Stars je alionekana wapi? hilo ndio lile la kiungo Henry Joseph alipoteuliwa Stars pasipo kuichezea klabu yake ya Simba ambayo ilimsajili akitokea Norway.

Uteuzi wa Kapombe unazua utata kwani ameshindwa kucheza soka la ushindnai kwa muda mrefu hivyo atapata vipi uzoefu wa kuwavaa Zimbabwe ambao wamepangwa kucheza na Stars mei 30 mwaka huku katika tiketi ya kuwania kufuzu hatua ya makundi mataifa Afrika.

TFF msikurupuke tu ili mradi mshangiliwe na mashabiki wa soka lakini Kapombe akija kukosea lawama nyingine zitawaandama, sina imani na kiwango cha Kapombe aidha kama kiko vile vile au kimeshuka, Ni hayo tu tukutane wiki ijayo.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA