LOGARUSIC AWAAHIDI USHINDI SIMBA KESHO

Kocha wa Simba, Zdavko Logarusic, amewatoa shaka mashabiki wa timu hiyo waliopoteza furaha kwa kuwaambia kuwa kipigo alichoipa Yanga katika pambano la Nani Mtani Jembe atakiendeleza kesho.

Simba na Yanga zitashuka uwanjani kesho kukabiliana katika moja ya mapambano ya hitimisho la Ligi Kuu Tanzania Bara litakalopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Simba, wameambulia patupu msimu huu baada ya Azam FC kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake, huku wapinzani wao, Yanga wakivuna nafasi ya pili.


Katika pambano la Nani Mtani Jembe lililopigwa Desemba 21 mwaka jana kwenye Uwanja wa Taifa, Simba iliichakaza Yanga kwa mabao 3-1.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu kutoka Zanzibar jana, Logarusic, alisema: “Nafahamu wapo mashabiki wetu ambao wamekata tamaa baada ya timu yao kuukosa ubingwa na hakika ni kitu kilichonisikitisha hata mimi, lakini niseme kwamba tutafurahi pamoja Jumamosi.

“Hawana sababu ya kuwa na presha kwa vile Yanga tuliyocheza nayo Desemba ndiyo hiyo hiyo tutakayocheza nayo Jumamosi sijaona kama imebadilika  kiasi ambacho iwe tishio kwa timu yangu.

“Nimewaambia wachezaji wangu huu ndiyo mchezo ambao tunatakiwa kuutumia kurudisha imani kwa mashabiki wetu, duniani kote ukiondoa ubingwa ambao kila mmoja anauhitaji, jambo jingine la maana ni kumfunga mpinzani wako, kitu ambacho sioni sababu ya sisi kushindwa.”

Alisema hahofii lolote hata kama kuna maneno kuwa atafukuzwa kwani kocha yeyote inabidi awe tayari kwa lolote, lakini amewaomba wachezaji wake waifunge Yanga kesho ili wasiaibike.

Kocha huyo mwenye vituko vingi awapo uwanjani anaamini timu yake itaibuka na ushindi mbele ya Yanga na kudai ukubwa wa majina ya wapinzani wao wala haumtishi kwani wanaingia uwanjani kusaka heshima, hivyo wachezaji wake hawapaswi kuwa na presha ya mchezo.

“Tumekosa vyote na tutaendelea kuwa watazamaji kwenye michuano ya kimataifa, tangu mwanzo tulipotea, hatukujipanga, lakini hatupaswi kuangalia hayo na sasa tunacheza mechi ya mwisho ili kusaka heshima tu.

“Wachezaji wanapaswa kujua hilo, ushindi katika mechi hii ni lazima na wala wasiwe na presha kwani mchezo huu ni wa kawaida, hivyo tutaingia tukiwa hatuna presha zaidi ya kutaka ushindi na kutunza heshima yetu kwani haitapendeza kama tutapoteza mchezo huu, tutaaibika, tukose hata nafasi ya nne?!

“Yanga ni timu kubwa na nzuri na imefanya vizuri msimu huu licha ya kukosa ubingwa, lakini hatupaswi kuogopa ukubwa wa majina ya wachezaji wao, tuko tayari kukabiliana nao,” aliongeza kocha huyo.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA