AZAM FC YAVURUGA MAPATO YA SIMBA NA YANGA

Kuibukia kwa mafanikio kwa timu ya Azam FC na kufanya vibaya kwa miamba ya soka nchini kumeanza kuzipa machungu ya kiuchumi timu za Simba na Yanga, ambazo katika mechi iliyopita baina ya watani hao wa jadi ziliingiza mapato kiduchu ya Sh. milioni 130, ambayo ni madogo zaidi kupatikana katika miaka ya karibuni tangu ulipojengwa uwanja mpya wa Taifa 2007.

Katika taarifa ya uongozi wa Simba iliyotolewa mwanzoni mwa wiki kuhusu tathimini yao kwa msimu huu, katibu mkuu wa klabu hiyo ya Msimbazi, Ezekiel Kamwaga alisema walikuwa wakiambulia mgawo wa mapato wa hadi Sh.300,000 katika baadhi ya mechi zao ikiwamo dhidi ya Ashanti United ambayo walilala 1-0.


Mechi baina ya Simba na Yanga ambayo kwa kawaida huwa na mashamsham tele nchi nzima, ya kufungia msimu huu ya Aprili 19, 2014 iligeuka kuwa kama mechi ya "ndondo" ikichezwa huku Azam ikiwa tayari imeshatwaa ubingwa wa bara kwa mara ya kwanza tangu ilipopanda daraja 2008.

Mashabiki wachache mno walihudhuria kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam katika mechi hiyo iliyokosa mvuto huku shamrashamra zikitawala "upande wa pili" kwenye uwanja wa Azam Complex ambako Azam walikuwa wakikabidhiwa kombe lao na kuwashuhudia mashabiki wote walioingia siku hiyo wakipewa chakula na vinywaji bure.

Mapato ya Sh. milioni 130 yaliyozishuhudia timu hizo kila moja ikiambulia mgawo wa Sh. milioni 30, yalikuwa ni pigo kiuchumi kwa timu hizo zinazotegemea kwa kiasi kikubwa mapato makubwa ya mechi baina yao kwa ajili ya "kuzibia mashimo" mengi katika kujiendesha kila msimu.

Kufikia sasa, rekodi ya mapato ya mechi baina ya Simba na Yanga ni ya raundi ya kwanza msimu huu iliyomalizika kwa sare ya 3-3 ambayo iliingiza Sh. milioni 500.7.

Rekodi ya awali ya mapato ya mechi baina ya miamba hao wawili wa soka nchini ilikuwa ni Sh. milioni 500.4, iliyopatikana katika mechi ya kufungia msimu uliopita ambayo Yanga ilishinda 2-0 Mei 18, 2013.

Kushuka kwa mapato katika mechi za Simba na zile za Yanga msimu huu kumechangiwa na kiwango kisichoridhishwa cha timu hizo zinazopendwa na mashabiki wengi zaidi nchini ambazo zitalazimika kujipanga zaidi msimu ujao ili kuwarejesha mashabiki wao viwanjani.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA