AZAM FC YAHAMISHIA MAKALI YAKE KLABU BINGWA AFRIKA

Baada ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu wa 2013/14, benchi la Azam FC limewapa likizo ya wiki saba wachezaji wake ili wapumzike kabla ya kuanza maandalizi ya msimu mpya wa ligi hiyo 2014/15 na mashindano ya kimataifa.

Azam FC imetwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa mara ya kwanza tangu ipande Ligi Kuu 2007 baada ya kumaliza kileleni ikiwa na pointi 62 ilizozipata bila kupoteza hata mechi moja kati ya mechi 26 zote za ligi.


Akizungumza katika mahojiano maalum mara tu baada ya kumalizika kwa mechi yao ya mwisho waliyoshinda 1-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Azam jijini Dar es Salaam juzi, Joseph Omog, kocha wa Azam FC, alisema nyota wake watapumzika kwa muda huo kabla ya kuingia kambini kujiweka sawa kwa ajili ya msimu ujao na mashindano ya kimataifa.

"Wachezaji wetu wamefanya kazi kubwa na wamechoka sana, itabidi wapumzike kwa wiki saba ili wapate nguvu ya kuanza maandalizi ya msimu ujao," alisema Omog.

"Tukisharejea, tutaingia kambini molja kwa moja tukianza na kambi ya ndani ya Tanzania lakini baadaye tutapiga kambi nje ya mipaka ya nchi hii ili tucheze mechi nyingi zaidi za kirafiki kabla ya kushiriki michuano ya Klabu Bingwa Afrika Februari mwakani," alisema zaidi raia huyo wa Cameroon.

Aidha, kocha huyo aliyewahi kutwaa taji la Kombe la Shirikisho barani Afrika akikinoa kikosi cxha Leopards ya Congo, alisema mwishoni mwa wiki hii atakwenda kwao Cameroon kwa mapumziko kabla ya kuanza maandalizi ya msimu mpya.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA