AIBU MABONDIA WA TANZANIA, WOTE WANUSURIKA KUUAWA

BONDIA Francis Miyeyusho amepigwa na mpinzani wake, Sukkassem Kietyongyuth wa Thailand kwa Knockout (KO) raundi ya kwanza sekunde ya 55 katika pambano la raundi 10 lisilo la ubingwa, uzito wa Feather lililofanyika ukumbi wa PTA, Temeke, Dar es Salaam usiku wa jumamosi.

Katika pambano hilo lililohudhuriwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam, Suleiman Kova aliyekuwa mgeni rasmi, Miyeyusho aligoma kupanda ulingoni kwa dakika zaidi ya 20 akishinikiza kwanza alipwe fedha zake.

Kamanda Kova ambaye mdogo wake, Mussa Kova ndiye aliyeandaa mapambano hayo kupitia kampuni yake ya Mawenzi Production, aliingilia sakata hilo na bondia huyo akalipwa fedha zake akapanda ulingoni.


Dalili za Miyeyusho ‘Chichi Mawe’ kupigwa zilionekana wakati nyimbo za taifa zinapigwa, kwani alikuwa asiyejiamini na mwenye kihoro, hivyo kumpa nafasi Mthailand kulianza kwa kasi pambano hilo.

Mgeni alianza kumtandika Miyeyusho tangu sekunde ya kwanza na ndani ya sekunde 20 bondia wa nyumbani alikaa chini akawahi kusimama, hata hivyo pigo hilo lilimuondoa mchezoni kabisa Chichi.

Mthailand aliibaini hali hiyo na akamfuata kwenye kamba Miyeyusho kumsukumia makonde mfululizo hadi refa Emmanuel Mlundwa alipokwenda kusimamisha pambano.

Refa alimpa nafasi Miyeyusho kuamua kuendelea au la na bondia huyo akajaribu kusogea mbele kurudi mchezoni, lakini akadondoka na Mlundwa akamaliza pambano, huku Chichi akisaidiwa na wasaidizi wake kuinuliwa chini kutolewa ulingoni.
 
Awali, Francis Cheka ‘SMG’ alitoshana nguvu na Gavad Zohrehvand wa Iran katika pambano lingine lisilo la ubingwa uzito wa Light Heavy raundi nane.

Hata hivyo, mashabiki walizomea matokeo ya sare katika pambano hilo, wakiamini Cheka alipoteza- kwani wazi mpinzani alionekana kutupa ngumi nyingi na raundi ya mwisho bondia wa Tanzania aliokolewa na kengele.

Ilionekana Cheka hakuwa na maandalizi mazuri kabla ya pambano lake la leo, kwani alikuwa ni mzito kutupa ngumi hadi kutembea ulingoni na alionekana kuanza kuchoka tangu raundi ya sita.

Katika mapambano ya utangulizi, Tasha Mjuaji alimshinda kwa pointi Steven Anastazi uzito wa Feather, Fabian Lyimo alimshinda Ramadhani Mnandi kwa pointi uzito wa Welter, Adam Yahya alimshinda kwa pointi Ramadhani Rajab uzito wa Light Fly na Sadik Momba alimshinda Epson John kwa pointi uzito wa Light, mapambano yote hayo raundi nne kila moja.
Ibrahim Class ‘Mawe’ alimshinda Mustafa Dotto kwa pointi pambano la raundi sita lisilo la ubingwa.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA