SCHOLES ATAKA MOYES APEWE MUDA MAN UNITED

David Moyes

Kiungo wa kati wa zamani wa Manchester United Paul Scholes ametoa wito kwa mabingwa wa Uingereza ambao wamekuwa wakihangaika wasimteme meneja David Moyes licha ya kichapo kingine cha aibu.

Wiki moja tu baada ya kushindwa 3-0 nyumbani na mahasimu wao wa jadi Liverpool, United walilazwa kwa maabo sawa debi ya Manchester nyumbani kwao Old Trafford Jumanne.

Edin Dzeko alifungia Manchester City la kwanza sekunde ya 43 na straika huyo wa Bosnian akaongeza jingine mapema kipindi cha pili kabla ya Yaya Toure kukamilisha kichapo hicho kwa bao la tatu dakika ya 90.

Kichapo hicho kiliacha United wakiwa nambari saba ligini na alama 12 nyuma ya Arsenal walio nambari nne.
Hayo yameacha mashabiki wakiwa na mshangao, kwamba kikosi kile kile kilichoshinda ligi msimu uliopita na meneja wa zamani Alex Ferguson kabla ya kustaafu, kimekuwa hakijiwezi hivyo dhidi ya timu za Uingereza kikiwa mikononi mwa raia huyo wa Scotland ambaye alichaguliwa na Fergie.


Lakini Scholes alisema kumlaumu meneja huyo wa zamani wa Everton litakuwa kosa, akisema United wanafaa kumuunga mkono meneja huyo zaidi soko litakapofunguliwa kuliko walivyofanya kipindi kifupi ambacho Moyes amekuwa Old Trafford.

"Lazima msimame naye. Alinunua wachezaji kadha ambao hawajafana lakini majira ya joto atahitaji usaidizi zaidi, hakuna shaka kuhusu hilo,” Scholes aliambia Sky Sports Jumanne.
"Je aliungwa mkono ilivyotakikana majira ya joto yaliyopita? Sina uhakika kuhusu hilo, lakini majira yajayo lazima aungwe mkono na nafikiri kwamba anajua anahitaji wachezaji,” akaongeza mchezaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Uingereza.

Nemanja Vidic anatarajiwa kuwaacha na kujiunga na Inter Milan mwisho wa msimu huku Rio Ferdinand na Patrice Evra wakiwa kwenye darubini.
Scholes alisema lazima Moyes aangazie kuimarisha safu ya ulinzi ya United, ingawa pia kumekuwepo wasiwasi kuhusu safu ya kati.

“Kwangu, inaonekana kuna ameneo kadha ambayo yanahitaji kuangazia,” Scholes, ambaye hatimaye alistaafu msimu uliopita, alisema.
"Sehemu ya kati ya safu ya kati unaweza kusema wamekuwa wakiangazia hilo kwa miaka kadha sasa na labda hawajapata jawabu mwafaka.

“Ninadhani ulinzi pia, ukizingatia kwamba Vidic anaenda – ni kama Rio na Evra pia wataenda, mabeki watatu kati ya wanne wako wanaenda – hiyo ni sehemu jingine ambayo anafaa kuangalia.
"Kwenda mbele, wako sawa. Lakini labda ni safu ya kati na ulinzi ambapo (Moyes) anafaa kuangazia.”

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA