REAL MADRID YAKALISHWA NA BARCELONA 4-3, MESSI ADHIHIRISHA UCHAWI WAKE

MSHAMBULIAJI Lionel Messi amepiga hat-trick usiku wa jana Barcelona ikishinda 4-3 dhidi ya Real Madrid katika mchezo wa La Liga uliofanyika Uwanja wa Santiago Bernabeu mjini Madrid.

Andres Iniesta alianza kuifungia Barcelona dakika ya saba, Karim Benzema akaisawazishia Real dakika ya 20 na kufunga la pili dakika ya 24.

Barcelona ikazinduka na kupata bao la kusawazisha dakika ya 42 kupitia kwa Messi, lakini Mwanasoka Bora wa Dunia, Cristiano Ronaldo akaifungia Real bao la tatu dakika ya 55 kwa penalti.

Messi akafunga mara mbili mfululizo kwa penalti dakika za 65 na 84 kukamilisha hat trick yake Barcelona ikifufua matumaini ya kutetea ubingwa wake msimu huu.


Real Ilimpoteza beki wake Sergio Ramos aliyetolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 63 kwa kumuangusha Neymar kwenye eneo la hatari, wakati Pepe, Di Maria, Alonso, Modric na Ronaldo wote walionyeshwa kadi za njano na kwa upande wa Barcelona, Fabregas na Busquets pia walionywa kwa kadi za njano.

Kwa matokeo hayo Real inabaki na pointi zake 70, ingawa inaendelea kuongoza La Liga kwa wastani wa mabao, ikiwa inalingana pointi na Atletico Madrid, ambayo mapema iliifunga Real Betis 2-0, mabao ya Gabi dakika ya 58 na Diego Costa 64, wakati Barcelona inabaki nafasi ya tatu licha ya kufikisha pointi 69. Barca na Real zimecheza mechi 28 kila moja, wakati Atletico imecheza mechi moja zaidi.
  
Kikosi cha Real Madrid kilikuwa: Diego Lopez, Pepe, Ramos, Cristiano Ronaldo, Benzema/Varane dk64, Bale, Marcelo, Xabi Alonso, Carvajal, Modric/Morata dk90 na Di Maria/Isco dk85.

Barcelona: Valdes, Alves, Piqué, Mascherano, Jordi Alba, Sergio, Xavi, Iniesta, Fabregas/Sanchez, dk78, Messi na Neymar/Pedro dk69.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA