ARSENAL NDEMBENDEMBE, YALALA 6-0 KWA VIDUME CHELSEA

GHARIKA. Jose Mourinho amempa mechi ya 1,000 chungu Arsene Wenger baada ya Chelsea kuigaragaza Arsenal mabao 6-0 katika mchezo wa Ligi Kuu ya England jana Uwanja wa Stamford Bridge, London.

Siku moja baada ya Wenger kukabidhiwa tuzo ya dhahabu kwa kuiongoza Arsenal katika mechi 1,000 tangu aanze kazi, jana alitoka Uwanja wa Stamford Bridge akiwa kichwa chini na asiye na hamu kwa kipigo kikali kutoka kwa wapinzani wao hao kwenye mbio za ubingwa.

Mcameroon Samuel Eto’o alitangulia kuifungia The Blues dakika ya tano kwa pasi ya Andre Schurrle, ambaye yeye mwenyewe akafunga la pili dakika ya saba kwa pasi ya Nemanja Matic kabla ya Edin Hazard kufunga kwa penalti dakika ya 17.


Penalti hiyo ilifuatia Alex Oxlade-Chamberlain kuushika mpira kwa makusudi akiokoa shuti la Edin Hazard, lakini ajabu refa akampa kadi nyekundu Kieran Gibbs.

Zikiwa zimesalia dakika tatu kabla ya mapumziko, Oscar aliifungia Chelsea bao la tatu kwa pasi ya Fernando Torres, ambaye naye alipokea krosi ya Andre Schurrle.

Kipindi cha pili, Chelsea walirudi na moto ule ule na dakika ya 66 Oscar aliifungia The Blues bao la tano kwa shuti la kawaida akiwa ndani ya eneo la hatari, ambalo lilionekana kama kipa Szczesny angeweza kuokoa, lakini akatunguliwa, kabla ya Mohamed Salah kufunga la sita dakika ya 71.

Kwa matokeo hayo, Chelsea inazidi kujiwekea zege kileleni kwa kutimiza pointi 69 baada ya mechi 31 na Arsenal inabaki na pointi zake 62 baada ya mechi 30.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA