ROONEY KUONGEZA MKATABA MAN UNITED

Wayne Rooney 

Wayne Rooney anatarajiwa kutia saini mkataba mpya wiki hii ambao utaweka straika huyo wa Uingereza katika Manchester United hadi mwisho wa msimu wa 2018-2019, vyombo vya habari nchini humo viliripoti Jumatatu.

Mchezaji huyo wa miaka 28 huenda atie saini mkataba huo Old Trafford Jumatano au Alhamisi, Chama cha Wanahabari kilisema.

Kumekuwepo na shaka kuhusu mustakabali wa Rooney katika miamba hao wa Ligi Kuu ya Uingereza hasa baada ya Chelsea kujaribu kumshawishi ajiunge nao kabla ya kuanza kwa msimu huu.

Licha ya masaibu ya United kwa sasa mbele ya meneja mpya David Moyes – ambayo yamepelekea wao kukwama nambari saba, alama 15 nyuma ya viongozi Chelsea – Rooney anadaiwa kutulia Old Trafford.


Mapema mwezi huu, Rooney alisisitiza kwamba “anaangazia uchezaji soka” huku uvumi ukitanda kuhusu mashauriano kuhusu mkataba wake, ambao unafikia kikomo mwisho wa msimu ujao.
Hata hivyo, alikiri kwamba ana azma ya kuvunja rekodi ya Bobby Charlton ya ufungaji mabao katika klabu. Charlton alifungia United mabao 249 na Rooney kwa sasa ana 208.

"Ni lengo kuu sana kwangu kujaribu kutimiza na kuvunja rekodi ya Sir Bobby, katika klabu na kimataifa,” alisema Rooney, ambaye amepungukiwa na magoli 11 pekee kuvunja rekodi ya Charlton aliyofungia Uingereza ambayo ni 49.”
"Ni jambo ambalo ningependa sana kufanya. Kama naweza kufanya hilo, ninaweza kujionea fahari sana, kwa sababu imedumu kwa muda mrefu.”

Rooney alianza uchezaji wake wa kulipwa akiwa na umri wa miaka 16 akiwa Everton chini ya Moyes na ametetea meneja huyo anayekabiliwa na shinikizo msimu wake wa kwanza, baada yake kushindwa kuendeleza ufanisi wa Alex Ferguson.

"David Moyes ni meneja mzuri ajabu," Rooney alisema wiki iliyopita.
"Nilifanya kazi naye nikiwa Everton na kwa miezi kadha hapa United. Amefanya kila awezalo, lakini wachezaji wake ndio wanaofaa kufanya zaidi na natumai kwamba tunaweza kufanya hilo.”

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA