MALINZI KUMLIPA POULSEN ILI AONDOKE

Rais  wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi, amesema atalipa nusu ya gharama zilizotokana na shirikisho hilo kuvunja mkataba wa aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu ya Taifa (Taifa Stars), Kim Poulsen.

Hata hivyo, Malinzi na Kim hawakutaka kuweka wazi hatua walizofikia baada ya kuamua kuvunja mkataba zaidi ya kueleza kuwa walifikia makubaliano ya pamoja.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Malinzi alisema sehemu nyingine ya gharama ya fedha zilizobakia zitalipwa na shirikisho hilo na waliamua kusitisha mkataba wa Kim ili wasake kocha mpya ambaye moja ya sifa zake ni kuwahi kuipeleka timu mojawapo ya Afrika kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika, AFCON.


Malinzi alisema serikali haihusiki na maamuzi hayo yaliyofikiwa na TFF ila ilijulishwa hatua zote za mchakato huo na kuelezwa tayari wameshaanza kusaka kocha atakayerithi mikoba ya Mdenmark huyo.

"Tulichokubaliana ni siri na kitabaki kuwa siri, TFF tutabeba, wapo wadau waliojitokeza kutulipia nusu kwa sababu waliahidi kuwa huu ni wakati wa mabadiliko," alisema Malinzi na baadaye kubadili kauli ya wadau na kujitaja yeye kuwa ndiye atakayelipa gharama hizo.

Aliongeza kwamba tayari TFF imeshabaki na majina matatu (hakuyataja) ya makocha ambao mmoja wao ataajiriwa akisema wawili wanatoka Uholanzi na mwingine ni raia wa Ujerumani.

"Jukumu lake kubwa litakuwa ni kuendeleza soka la vijana na atachagua msaidizi wake," aliongeza.

Alimtaja Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi, ambaye ana leseni Daraja A kuwa ndiye atakaimu nafasi ya Poulsen na ataiongoza Taifa Stars katika mechi moja itakayochezwa Machi 5 jijini Windhoek, Namibia.

POULSEN ANENA

Naye, Poulsen  aliwashukuru wachezaji, benchi la ufundi, wadhamini (Kampuni ya Bia Tanzania- TBL), mashabiki na wadau wote wa soka nchini kwa kumpa ushirikiano katika kipindi chote alichokuwa hapa nchini tangu Mei, 2012.

"Kunapokuja uongozi mpya lazima vitu kama hivi hutokea, uongozi mpya wa TFF umefanya mabadiliko mengi katika uongozi wake, hivyo hata mimi sishangai kuona nafukuzwa ingawa nimesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta mafanikio ya soka la Tanzania," alisema Poulsen.

Raia huyo wa Denmark alisema alikuta Tanzania ikiwa nafasi za chini katika viwango vya Fifa lakini sasa iko nafasi iko vizuri na ameiwezesha Taifa Stars kuzifunga timu ngumu za Zambia, Cameroon na Morocco.

"Kuna baadhi ya mechi tulifungwa kwa sababu ya mazingira yetu, mnakwenda kucheza  na timu ngumu huku wachezaji wenu hawana lishe ya uhakika, tuliangushwa na lishe katika mechi ya mwisho ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia," alisema Poulsen.

Alisema hata hivyo anaheshimu maamuzi ya viongozi wapya wa TFF ambao wanaamini wako sahihi.

Poulsen aliishukuru ajira aliyokuwa nayo Stars kwamba imemwezesha kupata kazi ya ukufunzi wa makocha wa FIFA na akaongeza atakuwapo nchini hadi atakapolipwa fedha zake.

Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Alfred Kidau, alisema idara yake iko wazi na mabadiliko yaliyofanywa kwenye benchi la ufundi yalikuwa ni ya nia njema.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA