MAKALA: RAGE ANAMALIZA UENYEKITI WAKE SIMBA, BILA MAKAMU MWENYEKITI.

Na Salum Fikiri Jr

SASA hivi hatuna haja ya kuangalia maigizo ya vichekesho kwenye luninga, siyo dili tena, ndio maana wasanii wa vichekesho wameanza kuipa kisogo fani hiyo, eti wanasema hailipi, ila hawajagundua kitu.

Kama inavyoelewa, Tanzania kila mtu msanii, mambo yote yanaenda kisanii tu, ukienda kwenye majukwaa ya kisiasa utavunjika mbavu mwenyewe, kiongozi tena waziri anahutubia wananchi na kuwaambia 'kama hamtaki kuleni nyasi, lazima ndege ya rais inunuliwe', maneno anayatoa baada ya wananchi kumuomba waziri asiidhinishe manunuzi ya ndege ya rais ambayo inagharimu mamilioni ya fedha.

Tuachane na hiyo, waziri mwingine aliwahi kuwaambia wananchi waogelee kwenye maji baada ya kushindwa kuwaletea kivuko kipya alichowaahidi, hiyo ni moja kati ya vunja mbavu ambazo tulikuwa tunazipata kwenye sanaa ya vichekesho pekee.

Msishangae kauli ya msanii mkongwe wa vichekesho nchini Amri Athuman 'King Majuto' kwamba anataka kuachana na maigizo na kwenda kujikita kwenye kilimo, maigizo hayalipi, kuna watu wameingilia anga zao.


Mwenyekiti wa klabu ya Simba Alhaj Ismail Aden Rage aliwahi kutoa matamko ya kuvunja mbavu, inafikia hatua maneno yake hayo ya kuchekesha yanatumika kwenye ringtone za miito ya simu, hii inadhihirisha yiongozi wetu wa kisiasa na nyanja nyingine wamejaa 'usanii'.

Wamechangia kuwamaliza wasanii wetu kama mzee Majuto na wengineo, sanaa zao si mali tena kama ilivyokuwa zamani, viongozi wetu wa zamani walijaa hekima, busara na ndio maana taifa lilisimama kwenye maadili.

Moja kati ya kauli za Rage zilizovunja mbavu watu wengi ni ile aliyoitoa kwenye mkutano mkuu wa wanachama wa klabu ya Simba uliofanyika Bwalo la Polisi, Rage akiwa kwenye ajenda ya saba aliwataka wanachama wake wasipige kelele kwani yeye anataka kuwahi mpirani.

'Nyie pigeni kelele mimi niko ajenda ya saba, watu tunataka kwenda kuangalia mpira', alisikika Rage, maneno hayo ni kama kichekesho, kwani kiongozi mwenye weledi awezi kuzungumzahuku wanaomsikiliza nao wanazungumza, inaonekana wazi kabisa Rage ameshindwa kuwatuliza wanachama wake na hawamuelewi.

Ukichana na kituko hicho, siku za hivi karibuni mwenyekiti huyo wa Simba alisimamishwa uenyekiti na kamati yake ya utendaji alipokuwa nje ya nchi kikazi, aliporejea nchini Rage aliitisha mkutano na waandishi wa habari katika makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo mtaa wa Msimbazi.

Katika mkutano huo Rage alipinga vikali kusimamishwa kwake katika nafasi hiyo na kuwaita waliofanya hivyo ni sawa na kutisha kikao cha harusi, moja kati ya kauli yake ya kuvunja mbavu inasikika mara kwa mara katika kituo kimoja cha redio cha jijini Dar es Salaam.

Kiundani juu ya maneno yake yanaonyesha kuwepo kwa ukiukwaji mkubwa wa katiba ya klabu ya Simba, katiba ya Simba inachezewa na kusababisha migogoro, kamati ya utendaji ya klabu ya Simba chini ya kaimu makamu mwenyekiti Joseph Itang'are maarufu mzee Kinesi ilitangaza kumsimamisha Rage.

Rage alisimamishwa na kamati yake baada ya kudaiwa kuisigina katiba, kamati hiyo ilimteua mzee Kinesi kuwa kaimu mwenyekiti badala ya nafasi yake ya mwanzo ya kaimu makamu mwenyekiti, pia Sued Mkwabi alitangazwa kuwa kaimu makamu mwenyekiti,

Mkwabi alichukua nafasi ya mzee Kinesi, uteuzi huo ulipokelewa kwa mikono miwili na wanachama wa klabu hiyo ambapo baadaye walianza harakati zao za kuimarisha kikosi, kamati hiyo iliwafuta kazi makocha Abdallah Kibadeni na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo.

Kisha ikasimamia kuimarisha benchi la ufundi tofauti na Rage ambaye alisimamia migogoro peke yake na kuwang'ang'ania makocha walewale ambao walishindwa kuipaisha Simba, kamati ya utendaji ilimsainisha mkataba wa miezi sita kocha wa zamani wa Gor Mahia ya Kenya Mcroatia Zdravko Logarusic.

Selema Matola kocha wa kikosi cha pili cha Simba, Simba B alipandishwa kuwa msaidizi wa kocha mkuu Logarusic au Loga, baadaye Simba ilifanya usajili wa kushtua, Yaw Berko kipa wa zamani wa Yanga alisaini mkataba wa miezi sita kuitumikia Simba.

Mbali na Berko, Simba ilimsajili kipa Ivo Mapunda na beki kisiki Donald Mosoti waliokuwa wakiichezea Gor Mahia ya Kenya, usajili huo uliweza kuleta faraja kwa mashabiki wa Simba, wakati kamati ya utendaji ya klabu ya Simba ikifanya vema, mwenyekiti aliyesimamishwa Ismail Aden Rage alikuwa akiangaika kutafuta suluhisho ili arejee katika kiti chake, Rage alibisha hodi TFF kuomba arejeshewe madaraka yake.

TFF kupitia kamati yake ya sheria, hadhi za wachezaji ilimrejesha Rage madarakani kwa masharti maalum, kamati hiyo ya TFF ilitengua maamuzi ya kamati ya utendaji ya klabu ya Simba ya kumsimamisha mwenyekiti wake.

TFF ilimtaka Rage kuitisha mkutano wa dhalula wa wanachama wote wa klabu ya Simba ukiwa na ajenda moja ya upatanishi ndani ya siku 14 na asingefanya hivyo hatua kali za kinidhamu zingechukuliwa dhidi yake, hata hivyo TFF ilimuomba Rage aitishe uchaguzi wa kumpata makamu mwenyekiti.

Nafasi ya makamu mwenyekiti katika klabu ya Simba haijazibwa kwa muda mrefu tangia aliyekuwa akishika wadhifa huo Gofrey Nyange 'Kaburu' kujiuzuru, Joseph Itang'are mzee Kinesi alichaguliwa kwa muda kuwa kaimu makamu mwenyekiti.

Tangia TFF ilipomtaka Rage aitishe mkutano ndani ya siku 14, bado hajafanya hivyo na wala hakuna dalili za kuwepo kwa uchaguzi wa kumpata makamu mwenyekiti.

Hivi karibuni Rage alitangaza kuwepo kwa mkutano wa wanachama wote wenye ajenda moja ya marekebisho ya katiba, mbali ya kuwepo malalamiko kutoka kwa wanachama wa klabu hiyo kutaka mkutano huo uongezewe ajenda, hakuna mabadiliko yoyote ya ajenda hadi sasa.

Kwa vyovyote vile Wanasimba wanakwenda kuipitia katiba yao kwa kuifanyia marekebisho kwenye vifungu kadhaa pasipo kuzungumzia kero nyingine zilizopo, kinachoniuma mimi ni ile nafasi ya makamu mwenyekiti kutozibwa.

Muda wa Rage kukaa madarakani unaelekea ukingoni kwa mujibu wa katiba, kukosekana kwa makamu mwenyekiti kunaonyesha wazi kuwepo kwa uvunjifu mkubwa wa katiba unaofanywa na uongozi wa Rage.

Kitu muhimu na hasa kilichotakiwa na kuzingatiwa na viongozi wa Simba ni matumizi sahihi ya katiba, katiba inapaswa kuheshimiwa na siku zote kiongozi bora ni yule anayeisimamia vema katiba.

Leo hii tunashuhudia madudu katika uongozi wa Simba uliochini yake  Ismail Aden Rage, ukiukwaji wa katiba usiendelee kushika hatamu kwa viongozi wajao katika klabu hiyo ya Simba ambayo inaheshimika katika ukanda huu wa Afrika mashariki na kati.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA