KOCHA WA YANGA AAPA KUIUMALIZA MAPEMA AL AHLY

Na Regina Mkonde, Bagamoyo

Kocha mkuu wa mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Yanga, Mholanzi Hans van der Pluijm, amesema atahakikisha anatumia mbinu zote alizo nazo ili kuiondoa Al Ahly ya Misri kwenye mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuifanya ajira yake iendelee kuwapo ndani ya Wanajangwani hao.

Akizungumza juzi jioni baada ya timu hiyo kufika Bagamoyo mkoani Pwani, Pluijm alisema aliufahamu 'mtihani' huo wa kukabiliana na Al Ahly mapema kabla ya kuja nchini kukubali ajira ya kuifundisha Yanga.

Pluijm alisema katika soka hakuna kitakachoshindikana na akaongeza dakika 180 ndizo zitakazoamua nani atasonga mbele.

Mholanzi huyo alisema katika dunia ya sasa kwenye soka hakuna mechi rahisi au mashindano mepesi na kwamba kila upande unajiandaa kufanya vizuri na kuweka rekodi.


"Najua sasa macho yote Yanga na wadau wengi wa soka wa Tanzania wanasubiri siku ifike, nilifahamu na nilianza mapema maandalizi ya kuwakabili hao mabingwa wa zamani wa Afrika, ila na mechi za ligi ya ndani ni muhimu na tutataka kushinda, " alisema kocha huyo.

Alieleza kwamba endapo wachezaji wake watakuwa 'fiti' ana hakika wataonyesha kiwango bora na hakuna atakayepata ushindi bila ya kupambana.

Aliongeza kuwa, kushinda katika mechi ya kesho ya ligi dhidi ya Ruvu Shooting kutawaongezea morali wachezaji wake ambao nao wanaiwaza Al Ahly.

Kama walivyofanya Al Ahly kuleta 'mashushu' wake kuipeleleza Yanga ilipokuwa inacheza na Komorozine ya Comoro katika mechi yake ya kwanza ya mashindano hayo ya kimataifa, wawakilishi hao pekee wa Tanzania waliobakia kwenye michuano ya Afrika, kocha msaidizi  Boniface Mkwasa, naye yuko jijini Cairo akiwasoma wapinzani wao.

Yanga ilisonga mbele katika mashindano hayo ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu baada ya kuitoa Komorozine kwenye hatua ya awali kwa jumla ya mabao 12-2.

Mshambuliaji wa Yanga, Mrisho Ngasa, ndiye anayeongoza kwa kupachika mabao katika mashindano hayo yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) baada ya kufunga hatrick mbili nyumbani na ugenini dhidi ya Wacomoro hao.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA