AZAM YAHAMISHIA HASIRA ZAKE LIGI KUU BARA.

AZAM FC sasa inaelekeza nguvu zake katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara baada ya jana kutolewa mapema katika michuano ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika.

Timu hiyo ya Alhaj Sheikh Said Salim Awadh Bakhresa na familia yake, yenye maskani yake Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, jana ilifungwa mabao 2-0 na wenyeji Ferroviario Beira kwenye Uwanja wa Ferroviario Beira mjini Beira Msumbiji katika mchezo wa marudiano, Raundi ya Awali, Kombe la Shirikisho.

Katibu Mkuu wa Azam FC, Nassor Idrisa ‘Father’ amesema kwamba matokeo hayo yamewaumiza, lakini wanalazimika kukubaliana nayo kwa sababu huo siyo mwisho wa maisha.


“Ni huzuni tu hapa, kuanzia kwa viongozi, wachezaji, benchi la Ufundi na wote katika msafara wetu. Lakini tunafarijiana hivyo hivyo, huu si mwisho wa maisha, kama kuna sehemu tulikosea, basi tumepata somo na tutajirekebisha,”alisema Father.

Alisema kwamba timu inarejea leo Dar es Salaam kuendelea na mazoezi kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu, dhamira ikiwa ni kutwaa ubingwa na kufuta machungu ya matokeo ya michuano ya Afrika.

Imetuuma, lakini ndiyo soka; Katibu wa Azam FC, Nassor Idrisa 'Father' kushoto akiwa na kiongozi mwingine wa Azam FC, Abubakar Mapwisa kushoto
“Tulitengeneza nafasi nyingi za kufunga Dar es Salaam, lakini tukafunga bao moja tu, hilo ndilo lililotugharimu, ila  si vibaya ndiyo soka, sisi wa Azam ni kitu kimoja, tunashikamana na wachezaji wetu na kwa pamoja na tunaelekeza nguvu zetu kwenye Ligi Kuu,”alisema.

Aidha, Father aliwaomba radhi mashabiki na wapenzi wa Azam FC na kuwataka wawe wavumilivu, kwa kuwa dhamira ipo ya kufanya vyema kwenye michuano ya Afrika, basi iko siku nafsi zao zitafarijika.

Katika mchezo wa jana, uliofanyika sambamba na mvua kali iliyoharibu mandhari ya Uwanja, wenyeji walipata bao moja kila kipindi, yote yakifungwa na mshambuliaji wake hatari, Mario Simamunda dakika ya tano na ya 70.

Matokeo hayo yanaifanya Azam itolewe kwa jumla ya mabao 2-1 baada ya awali kushinda bao 1-0 mjini Dar es Salaam, bao pekee la mshambuliaji Kipre Herman Tchetche Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
  
Aidha, matokeo hayo pia yanamaanisha, Azam imeshindwa kufikia rekodi yake ya mwaka jana katika michuano hiyo, ilipotinga hatua ya 16 Bora na kutolewa na AS FAR Rabat ya Morocco chini ya kocha Muingereza, Stewart John Hall, aliyejiuzulu Septemba mwaka jana.

Matokeo hayo pia, yanamaanisha kocha Mcameroon Joseph Marius Omog ameshindwa kuendeleza rekodi yake nzuri aliyotoka nayo Kongo Brazaville, akiiwezesha Leopard FC kutwaa Kombe la Shirikisho.

Azam FC inaongoza Ligi Kuu ya Bara kwa pointi zake 36, ikifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga SC wenye pointi 35 sawa na Mbeya City iliyo nafasi ya tatu, wakati Simba SC yenye pointi 32, ipo nafasi ya nne.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA