ASKARI WA JKT WAUA SIMBA TAIFA, LAMBALAMBA YALAMBWA NA ASKARI MAGEREZA.

SIMBA SC imelambwa mabao 3-2 na JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Azam FC imelazimishwa sare ya kufungana mabao 2-2 na Prisons ya Mbeya Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.

Matokeo hayo yanamaanisha, Yanga SC iliyoshinda 7-0 dhidi ya Ruvu Shooting jana Uwanja wa Taifa, inaendelea kuongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 38, Azam ya pili 37 na Mbeya City ya tatu 35 na Simba SC ya nne 32.

Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam hadi mapumziko JKT Ruvu walikuwa mbele kwa mabao 2-0 yaliyotiwa kimiani na Hussein Bunu dakika ya 14 na Emmanuel Swita dakika ya 44 kwa penalti, baada ya Henry Joseph kumuangusha Amos Mgisa kwenye eneo la hatari.


Hata hivyo, penalti hiyo ilionekana kuwa ya utata, kwani mguu wa Henry ulionekana kwenda kuuondosha mpira miguuni mwa Mgisa bila kumgusa mchezaji huyo.

Kipindi cha pili, JKT Ruvu ilionekana kurudi na moto wake tena na kufanikiwa kupata bao la tatu mapema dakika ya 52, mfungaji Emmanuel Swita tena kwa shuti kali baada ya pasi ya Amosi Mgisa.

Simba SC ilizinduka baada ya  bao hilo na kupambana hadi kupata mabao mawili yaliyofungwa na Mrundi Amisi Tambwe dakika za 64 kwa penalti baada ya Amri Kiemba kuangushwa kwenye eneo la hatari na dakika ya 84, akiunganisha krosi ya Kiemba.

Uwanja wa Azam Complex, hadi mapumziko hakukuwa na timu iliyopata bao, lakini kipindi cha pili, Prisons walikuwa wa kwanza kupata bao lililofungwa na Omega Seme anayecheza kwa mkopo kutoka Yanga SC dakika ya 47 kwa shuti la mpira wa adhabu baada ya Aggrey Morris kumchezea rafu Jimmy Shoji.

Aggrey Morris akaisawazishia Azam FC dakika ya 50 kwa kichwa baada ya kuuwahi mpira uliorudishwa na beki wa Prisons kufuatia John Bocco kuunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu wa Erasto Nyoni.

Azam FC walionekana kuwa katika nafasi ya kuondoka na pointi tatu baada ya Kipre Herman Tchetche kuifungia bao la pili timu hiyo dakika ya 51 kwa shuti kali baada ya kuiwahi pasi ndefu ya Nyoni.

Kipre Tchetche alitolewa nje kwa kadi nyekundu dakika ya 58 baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na refa Alex Mahagi wa Mwanza kwa kuushika mpira makusudi ili kuuweka sawa.

Hata hivyo, zikiwa zimesalia dakika mbili mchezo huo kumalizika, Laurian Mpalile aliisawazishia Prisons dakika ya 88 baada ya pasi nzuri ya Freddy Chudu.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA