AMISSI TAMBWE, HAWEZEKANIKI TENA KWA MABAO.

Na Salum Fikiri Jr

KAMA kuna kosa kubwa lilifanywa na uongozi wa Simba ni pale ulipoamua kumuuza mshambuliaji wake ghali na wa kimataifa Mganda Emmanuel Okwi kwa waarabu wa Etoile Du Sahel ya Tunisia na kuibua maswali kadhaa kwa mashabiki wa soka.

Simba ilifanya kosa hilo ambalo mpaka sasa limeweza kuiatihili, Simba ilipoteza mwelekeo baada ya kuondoka mshambuliaji huyo ambaye alikuwa mwiba mchungu kwa timu pinzani hasa Yanga.

Yanga hawatamsahau Okwi kwa vile ndiye aliyeandikisha rekodi ya ushindi wa mabao 5-0 ambao mpaka sasa bado unawatesa, katika ushindi huo wa kihistoria Okwi aliweza kufunga magoli mawili huku akisaidia kutengeneza mengine matatu.

Bosi wa Yanga Yusuf Manji alitumia kila njia kuhakikisha anampata Okwi, ni kweli yametimia kwa licha ya uongozi wa Simba kumuuza kwa Etoile Du Sahel ya Tunisia, Yanga ilitumia njia ya mkato na kumnasa mshambuliaji huyo.


Ingawa usajili wake umezua utata, lakini imefanikiwa baada ya shirikisho la kandanda duniani Fifa kuthibitisha usajili wake kwa klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Jangwani, Fifa ilitoa ufafanuzi huo baada ya kuombwa na shirikisho la kandanda nchini TFF ambalo liliusimamisha usajili wa Okwi Yanga.

Tangia Okwi alipoondoka katika kikosi cha Simba amesababisha timu hiyo kukosa mbadala wake kwa kipindi kirefu na kupelekea timu hiyo kuvuliwa taji lake la ubingwa wa bara na mtani wake wa jadi Yanga, pia Simba iliondolewa katika michuano ya kimataifa kwa aibu.

Okwi alikuwa msaada muhimu katika kikosi hicho ambapo baadaye wanachama wa timu hiyo walianza kumnyooshea vidole mwenyekiti wao Ismail Aden Rage kwamba anaihujumu Simba kichinichini, mgogoro huo ulisababisha kamati ya utendaji kumsimamisha uenyekiti Rage.

Mpaka shirikisho la kandanda nchini TFF lilipoingilia kati mgogoro huo, Lakini TFF iliamua kuingilia kati mgogoro huo baada ya wajumbe wa kamati kumsiamisha kimakosa mwenyekiti huyo, pia TFF iliamua kulivalia njuga sakata la Okwi ambaye aliuzwa Etoile Du Sahel ya Tunisia.

Katika mauzo hayo Simba haijalipwa fedha zao hadi leo huku Okwi akihama timu moja kwenda nyingine mara akatua Yanga ya Tanzania, kitendo hicho nacho kiliibua mjadala mzito uliosababisha Okwi kusimamishwa na TFF.

Amani kwa sasa katika klabu ya Simba imetulia, hakuna tena mgogoro wa uongozi wala wachezaji, timu ilikuwa inacheza pasipo maelewano kwa sababu haikuwa na straika wala kiungo mchezeshaji, tangia kuondoka kwa Okwi safu ya ushambuliaji ya Simba ilipwaya.

Hivyo iliwaudhi mashabiki wake ambapo wameishuhudia mara kadhaa ikipoteza magoli ya wazi huku safu yao ya ulinzi ikiruhusu magoli ya kizembe, Usajili uliendelea ili kupata mbadala.

Hatimaye suluhisho limepatikana, Wekundu wa Msimbazi wamefanikiwa kupata mshambuliaji wa kati ambaye si mwingine ni Amissi Tambwe raia wa Burundi, Ujio wa Tambwe katika klabu ya Simba kumeweza kurudisha imani kwa mashabiki wake kwani safu ya ushambuliaji ya Simba imeanza kutisha.

Simba imeanza kuwa moto wa kuotea mbali hasa katika idara zake zote kuanzia ulinzi, kiungo hadi ushambuliaji, ushirikiano kati ya mabeki na washambuliaji umeifanya timu hiyo kuingia katika vita kali ya kuwania ubingwa dhidi ya Azam FC, Yanga na Mbeya City.

Vigogo hivyo viko katika nafasi za juu zikipigania ubingwa wa bara, Amissi Tambwe ametokea kuwa mfungaji mahiri kwa upande wa Simba ambapo mara kadhaa ametokea kuipa ushindi ama kuinusuru isifungwe.

Majuma mawili yaliyopita Simba ilikuwa na mechi zake mikoani, Simba ilielekea mikoa ya Morogoro, Tanga na Mbeya ambapo ilicheza na wenyeji wake Mtibwa Sugar, Mgambo JKT na Mbeya City, katika mechi hizo kikosi cha Simba kilikutana na usindani mkali ambapo iliambulia pointi mbili tu.

Ilianza kwenda sare na Mtibwa Sugar ya Morogoro ambapo zilifungana 1-1, Mtibwa ikiwa katika uwanja wake wa nyumbani ilitangulia kufunga goli lake la kuongoza likiwekwa kimiani na Mussa Hassani Mgosi, hata hivyo Amissi Tambwe aliiokoa Simba baada ya kuisawazishia.

Simba ilipoteza mchezo wake wa pili dhidi ya Mgambo JKT uliofanyika uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga ambapo ililala 1-0, lakini iliambulia pointi moja mbele ya Mbeya City ambapo zilitoka sare ya kufungana 1-1.

Katika mchezo huo vijana wa Mbeya City walitangulia kwa kufunga goli la kwanza lakini vijana wa Simba wanaonolewa na Mcroatia Zdravko Logarusic walisawazisha katika kipindi cha pili, goli la kusawazisha lilifungwa na Amissi Tambwe.

Tambwe ndio suluhisho la mabao katika kikosi cha Simba, Wanasimba wameanza kumsahau Emmanuel Okwi ambaye alikuwa nyota katika kikosi hicho, uwepo wa Tambwe unaipa kiburi Simba hata inapocheza na Yanga, kwani katika siku za hivi karibuni Simba iliifunga Yanga mabao 3-1 huku Tambwe akifunga magoli mawili.

Uwezo wa mshambuliaji huyo kwa kupachika magoli unafananishwa na enzi za Zamoyoni Mogella 'Golden Boy' ambaye alitisha kwa upachikaji magoli enzi zake, Tambwe anaongoza kwa upachikaji magoli katika ligi kuu ya Tanzania bara msimu huu hadi sasa amepachika mabao 15 huku anayemfuatia ana magoli 10.

Kwa kasi hii ya ufungaji, Tambwe anaweza kuvunja rekodi ya mabao ya Mohamed Hussein 'Mmachinga' ambaye alifikisha magoli 22 katika msimu mmoja, inawezekana Mrundi huyo akaifikia rekodi hiyo na kuivunja kabisa.

Tambwe ni msimu wake wa kwanza kuichezea Simba, aling'ara na klabu ya Vital'O ya Burundi katika michuano ya klabu bingwa Afrika mashariki na kati iliyofanyika mwaka jana Darfur, Sudan ambapo timu za Tanzania zilijitoa.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA