YANGA YAIPISHA AZAM KILELENI, KIPRE TCHETCHE HATARI.

Mabingwa Yanga walishikwa kwa sare ya 0-0 ugenini mkoani Tanga dhidi ya Coastal Union na kushuhudia wakitema uongozi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya Azam FC kushinda 1-0 dhidi ya Rhino Rangers na kushika usukani wa ligi.

Mbeya City ambao waliianza siku ya jana wakiwa na pointi 30 sawa na Azam, nao walidondosha pointi mbili jana kufuatia sare ya 1-1 ugenini Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini.

Matokeo hayo yalimaanisha kwamba Azam sasa wako kileleni mwa msimamo wakiwa na pointi 33, moja juu ya Yanga walio katika nafasi ya pili, huku Mbeya City wakibaki katika nafasi yao ya tatu wakiwa na pointi 31.


Simba walio katika nafasi ya nne wakiwa na pointi 27, wanayo fursa ya kusogea hadi pointi tatu nyuma ya vinara Azam kwa ushindi dhidi ya JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kesho.   

Mfungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita Kipre Tchetche alifunga bao lake la 9 katika dakika ya 31 jana na hivyo kubakisha goli moja kumfikia kinara Amisi Tambwe wa Simba wakati alipoisaidia Azam kupanda kileleni kwenye Uwanja wa Azam Complex. 

Ruvu Shooting walitangulia kupata goli kupitia kwa Jerome Lambele katika dakika ya 4 lakini Mbeya City ambayo pamoja na Azam ndizo timu pekee ambazo hazijapoteza mechi hadi sasa, ilisawazisha kupitia kwa Deus Kaseke dakika kumi baadaye.

Mkoani Tanga, Yanga walianza kwa kasi wakapata kona tatu ndani ya dakika tano za mwanzo lakini hazikuzaa matunda kutokana na umahiri wa kipa wao wa zamani Shaban Kado aliyepangua pia mashuti ya winga Mrisho Ngasa na kiungo Haruna Niyonzima 'Fabregas'.

Katika dakika ya 29 mpira ulilazimika kusimama kwa dakika moja kupisha uokotaji wa chupa za maji zilizorushwa na mashabiki walioaminika kuwa Yanga waliochukia baada ya refa msaidizi namba moja John Kanyenye wa Iringa kukataa kuwapa penalti baada ya mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbagu kumnawisha mpira beki wa Coastal, Juma Nyoso ndani ya boksi. Hata hivyo, Kavumbagu alifanya faulo kabla ya tukio hilo kwani alinyanyua mguu wakati Nyoso akitaka kupiga kichwa.

Dakika tisa baadaye, mashabiki wa Coastal walijibu mapigo kwa kurusha chupa za maji langoni mwa Yanga baada ya timu yao kufanya shambulizi kali la kushtukiza. Mpira pia ulisimama kwa dakika moja kupisha uokotaji wa wa chupa hizo.

Yanga walifanya mashambulizi hatari 13 kipindi cha kwanza yaliyozaa kona nane huku wenyeji wao wakifanya mashambulizi matatu makali ya kushtukiza na yaliyompa wakati mgumu kipa Deogratius Munishi 'Dida' kuokoa.

Coastal walibadilika kwa kiasi kikubwa kipindi cha pili wakisaidiwa na upepo mkali uliokuwa unavuma kutoka Kaskazini kuelekea lango la Yanga na kuwachanganya wachezaji wa Yanga hadi kufikia hatua Cannavaro kumsukuma Niyonzima katika dakika ya 73.

Baada ya mechi hiyo, kocha wa Yanga, Hans der Pluijm, alisema: "Tulipoteza mechi kipindi cha kwanza tuliposhindwa kupata bao licha ya kutengeneza nafasi nyingi. Kipindi cha pili tulishindwa kucheza mpira mzuri kutokana na upepo mkali."

Kocha wa Coastal, Mkenya Yusuph Chiko alisema: "Ni jambo jema tumepata pointi na hatujapoteza mechi tulicheza vizuri kipindi cha pili lakini bado tuna upungufu katika kuzitumia nafasi tunazotengeneza. Tutalifanyia kazi suala hili."

Vikosi Tanga vilikuwa; Coastal Union: Shaban Kado, Hamad Juma, Abdi Banda, Juma Nyoso, Mbwana Bakari, Jerry Santo, Daud Liyanga, Chrispin Odula, Lutimba Yayo/ Mohamed Miraji (dk. 88), , Haruna Moshi na Keneth Masumbuko/ Mohamed Sudi (dk. 78).

Yanga: Deogratius Munishi, Mbuyu Twite, Oscar Joshua. Nadir Haroub, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa/ Nizar Khalifani (dk. 83) na David Luhende/ Jerry Tegete (dk 66).

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA