LOGA AIPONDA FOWADI SIMBA, AZIDI KUMUANDAMA MWOMBEKI.

 Baada ya kupata ushindi finyu katika mechi yake ya kwanza katika Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara, Kocha Mkuu wa Simba, Zdravko Logarusic 'Loga', amesema ligi hiyo ni ngumu na timu ndogo ndizo zimekuwa kikwazo kwa klabu kongwe za hapa nchini, lakini akaweka wazi kuwa washambuliaji wake bado hawajaelewa darasa lake.

Simba juzi iliifunga Rhino Rangers ya mkoani Tabora bao 1-0 lililoiwezesha kufikisha pointi 27, hivyo kuendelea kukaa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi hiyo inayoongozwa na wapinzani wao Yanga wakifuatiwa na Azam FC na Mbeya City.


Akizungumza juzi baada ya mechi, Loga, alisema mechi yao ilikuwa ngumu na ushindi huo finyu walioupata umethibitisha kwamba hakuna timu ya kuidharau katika ligi.
Loga alisema kikosi chake kilikutana na ushindani na kupoteza nafasi nyingi za kufunga ambazo walitengeneza katika mchezo huo.

"Ligi ina ushindani, ina changamoto na si rahisi, kila timu sasa ni kubwa, leo (juzi) nimethibitisha timu ndogo zinavyoendelea kuzisumbua timu kongwe. Jambo zuri nimefurahi ni kupata ushindi," alieleza kocha huyo raia wa Croatia.

Loga alisikitishwa pia na kitendo cha wachezaji wake kukosa nafasi za kufunga na kueleza kwamba hali hiyo inatokana na kikosi chake kutokuwa na washambuliaji wenye uzoefu.

Alisema anatarajia katika mechi ijayo kuwaanzisha Edward Christopher na Zahor Pazi.
Hata hivyo, wakati Loga akieleza hayo, mshambuliaji wa Simba, Amisi Tambwe ndiye anayeongoza katika orodha ya wafungaji kwenye ligi hiyo.

AMCHAMBUA MWOMBEKI


Loga alisema hataweza kuvumilia kuona mchezaji anabaki uwanjani akifanya 'madudu' na si yale aliyoelekezwa katika benchi la ufundi kabla ya kuingia kucheza.

Kocha huyo alisema mchezaji anayecheza kwa kufuata maelekezo ataendelea kumpa nafasi kwa sababu malengo yake kila mechi ni kushinda.

"Sina ujamaa na mtu, wao ni wachezaji na mimi ni kocha, anayefanya vizuri atabaki uwanjani na atakayeharibu nitamtoa nje, hii ni katika kujenga uimara wa kikosi changu kwenye kila idara," Logarusic aliongeza.

Betram Mwombeki aliingia katika dakika ya 65 akichukua nafasi ya Tambwe lakini zikiwa zimebakia dakika nne mchezo kumalizika alimtoa nje kutokana na kuboronga, hivyo kumpisha kiungo, Henry Joseph.

Simba itaanza tena mazoezi leo kwa ajili ya kujiandaa na mechi yake dhidi ya JKT Oljoro itakayofanyika Februari Mosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA