MZUNGU WA SIMBA ATOWEKA.

Baada ya kuipa timu yake ushindi wa mabao 3-1 katika mechi ya kirafiki dhidi ya Yanga (Nani Mtani Jembe), Kocha Mkuu wa Simba, Zdravok Logarusic 'Loga', aliondoka nchini jana usiku na kwenda kwao Croatia kwa ajili ya mapumziko ya Sikukuu ya Krismasi na mwaka mpya huku akiahidi makubwa zaidi atakaporejea.

Mcroatia huyo atakosa mechi mbili za hatua ya makundi katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi yatakayofanyika kuanzia Januari Mosi mwakani.

Logarusic aliyewahi kuifundisha Gor Mahia ya Kenya, Jumamosi aliiongoza Simba kwa mara ya kwanza wakati ikiibuka na ushindi huo mnono dhidi ya watani zao Yanga.


Akizungumza na gazeti hili jana mchana, Logarusic, alisema ushindi wa Jumamosi ni mwanzo wa mafanikio ambayo Simba itayapata katika msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara unaotarajiwa kuendelea tena kuanzia Januari 25, mwakani.

Logarusic alisema mechi hiyo ilikuwa ngumu kwake katika dakika 15 za kwanza kwa sababu alihitaji muda wa kuwasoma wapinzani wake na kuimarisha kikosi chake haraka pale alipobaini kuna upungufu.

Alisema bado anahitaji muda zaidi wa kuwaimarisha wachezaji wake lakini akasisitiza kuwa, mashabiki na wanachama wa Simba watafurahi msimu huu.

"Kila mechi ina ushindani wake na mipango yake, kikubwa ni kumsoma mpinzani wako na kujipanga kumkabili, ndivyo nilivyofanya na nilifanikiwa," alisema Logarusic.

Aliongeza kwamba anaondoka lakini ameacha programu ya mazoezi itakayokuwa chini ya kocha msaidizi, Selemani Matola.

Matola aliuambia mtandao huu kwamba wachezaji wao wamewapa mapumziko mafupi na watarejea tena kuanza mazoezi Ijumaa.

Alisema kila mchezaji ana maagizo binafsi aliyoachiwa na kocha mkuu ili kulinda viwango vyao.

"Tunamshukuru Mungu tulipata ushindi jana (juzi), sasa vijana wako katika mapumziko, ila kocha mkuu amenipa programu ya mazoezi tutakayoifuata katika kipindi ambacho hatakuwapo," Matola alieleza.

Mabao ya Simba katika mechi ya juzi yalifungwa na Amisi Tambwe aliyepachika mara mbili na la tatu likiwekwa nyavuni na kiungo wao mpya, Awadh Juma wakati la Yanga likifungwa na na Mganda, Emmanuel Okwi.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA