MAKALA: NI NDOTO VIJANA KUPATA NAFASI YANGA, SIMBA AU TAIFA STARS.

Na Prince Hoza


AKILI za wapenda soka walio wengi hapa nchini ni kuona soka la vijana likipewa nafasi, vijana wanapewa nafasi ili waweze kuisaidia nchi katika siku za usoni baada ya kaka zao kutundika daruga, lakini pia vijana ni mchango mkubwa kwenye maendeleo ya nchi.

Lakini jitihada zake zinashindikana, sioni kama kuna dalili za kuwaamini vijana, katika siku za hivi karibuni neno vijana limegeuka siasa kwenye vilabu vyetu vya soka hasa Yanga, Simba na Azam pia limehamia kwenye timu ya taifa, Taifa Stars.

Nimeamua kuandika ili kila Mtanzania ashuhudie mwenyewe jinsi mipango ya kutokomeza soka la vijana inavyozidi kuchukua kasi, mashabiki wa soka nchini nao wanahusika kwa namna moja ama nyingine kutokomeza maendeleo ya soka la vijana.


Mambo mengi yanayotokea sasa ambayo yamezusha migogoro tena mikubwa katika vilabu vya soka sana sana yanachochewa na kuwemo vijana, Simba SC iliamua kuwapa nafasi chipukizi wake watano msimu uliopita kisha ikawapandisha wote.

Iifanya hivyo kufufatia ujio wa kocha Mfaransa Patrick Liewig, Liewig alikuja na falsafa ya kuendeleza soka la vijana kama alivyozoeleka kila anapokwenda kufundisha soka anapenda zaidi kutumia vijana, alifanya hivyo alipokuwa Ivory Coast ambapo aliinoa timu ya Asec Mimosas.

Liewig alikuwa na mipango thabiti ya kutumia vijana katika klabu ya Simba, lakini alianza kuandamwa kwa jicho la tatu, tatizo la vilabu vyetu ni kutaka mafanikio ya haraka, Washabiki wa Simba wanataka mafanikio ya haraka hasa kuiona timu yao inatwaa ubingwa wa bara huku ikimfunga mtani wake Yanga.

Ndivyo ilivyo kwa Yanga nayo inataka mafanikio ya haraka hasa kubeba ubingwa wa bara na kumfunga mtani wake Simba huku ikishindwa kuweka matumaini ya kushiriki michuano ya kimataifa, kushindikana kwa soka la vijana kwenye vilabu hivi tatizo kubwa ni mafanikio ya haraka.

Soka la Tanzania litachukua muda kupiga hatua kutokana na siasa zinazoendelea hasa za kutowahitaji wachezaji chipukizi, hilo linatokana na nini unajua kila kiongozi wa klabu kubwa kitu muhimu kwake ni kuona ushindi unapatikana.

Siku zote wachezaji chipukizi wanacheza kwa malengo, ushindi si kitu muhimu kwao zaidi ya kujifunza kisha baadaye kuelewa na kuanza kuweka mikakati ya ushindi, sasa hilo haliwezekani kwa Simba na Yanga ambao ndoto zao ni kucghukua ubingwa wa bara au kumfunga mtani wake.

Ndio maana imekuwa ngumu kusajiliwa chipukizi badala yake majina makubwa yatazidi kuonekana kwenye vilabu hivyo, Tunmeshuhudia usajili wa Emmanuel Okwi katika klabu ya Yanga, ile ilikuwa nafasi ya kumuongeza chipukizi mmmoja kutoka kikosi cha pili kilichotoka kushiriki Uhai Cup.

Kikosi cha Yanga B kilishiriki michuano ya UNhai Cup na kuingia fainali ambapo ilicheza na Coastal Union, Licha ya kufungwa katika fainali lakini Yanga ilionyesha uwezo wa hali ya juu na wala haikubebwa kufikia hatua hiyo, umuhimu wa vilabu hasa zinazoshriki ligi kuu kutumia vikosi vyao vya pili lengo ni kuimarisha timu zao.

Timu hizo zinaruhusiwa kuwatumia wachezaji wao wa vikosi vya pili pindi zinapohitaji kufanya hivyo, lakini imekuwa ngumu kwa timu hizo kuwatumia wachezaji wao wa timu B, Simba ilijaribu kufanya hivyo msimu uliopita lakini ikaja kumtimua kocha wake Patrick Liewig kwa madai timu ilifanya vibaya.

Ikiwa na kikosi chake cha pili Simba ilikamata nafasi ya nne nafasi ambayo ilionekana mbaya kwa upande wao, lakini ilikusanya vijana wengi, lawama mbalimbali zilianza kutolewa na kundi la mashabiki wao wakitaka timu iongezewe nguvu kwa kusajili wachezaji wenye uzoefu badala ya kuwaacha vijana wao wapate uzoefu.

Badala yake ikampa ajira kocha mzawa Abdallah Kibaden na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo 'Julio', matumaini ya Wanamsimbazi yalibaki kwa makocha hao wazalendo ambao waliaminiwa kwa falsafa yao, Kibadeni aliahidi mafanikio makubwa kwa kikosi chake na kutaka kiongezewe nguvu.

Malengo yao yalikuwa mazuri ambapo waliwaacha wakongwe na kuwapandisha chipukizi wote waliofanya vizuri katika michuano ya Uhai Cup na mingineyo, Simba ikawasajili nyota kadhaa ili kusaidiana na chipukizi hao, na ilimaliza ligi ikiwa ya nne kama msimu uliopita.

Nafasi hiyo imeleta kizaazaa kilichopelekea kutimuliwa kwa makocha hao na nafasi yake kuchukuliwa na Mcrotia Zdravkos Lugarusic ambaye ameanza kazi ya kuionoa timu hiyo, lakini sioni dalili za kuwapa nafasi tena vijana katika kikosi hicho.

Tayari Simba imesajili nyota wapya watano katika usajili mdogo uliofunguliwa Novemba 15 na kufungwa Desemba 15  mwaka huu, katika usajili huo Simba imewasajili makipa Yaw Berko, Ivo Mapunda ambao waliwahi kuichezea Yanga huko nyuma.

Wngine ni Donald Musoti, Badru Ally na Awadh Juma, kusajiliwa kwa wachezaji hao kunahatarisha uwepo wa vijana katika kikosi hicho, Wakati Simba ikimlalamikia kipa wake Mganda Abel Dhaira nilifikiria kwamba nafasi yake itachukuliwa na kipa wake kutoka timu ya vijana Abou Hashimu atachukua nafasi.

Abou alifaa kuziba nafasi ya Dhaira, lakini ujio wa Berko na Mapunda unaweza kuhatarisha maisha ya kijana huyo katika klabu ya Simba, hii ndio sababu ya kuangamia soka la vijana nchini, mashabiki wanafurahia ujio wa Mapunda na Berko hawajui athali ya soka la vijana wao.

Na ndio maana timu ya taifa ikijaribu kufanyiwa marekebisho ya wachezaji na kuwekwa vijana badala ya wakongwe utasikia kocha hafai, timu haiwezi kwenda kokote nafasi ile angewekwa fulani ambaye ni mkongwe, usajili wa Okwi Jangwani unaungwa mkono na mashabiki wake pande zote za nchi.

Napigiwa simu mara zote nikiuliziwa ujio wake, lakini naona kama wauaji wakubwa wa soka la vijana, kama Yanga ilihitaji mshambuliaji kwanini isingempandisha kijana wake Masasi aliyeisaidia Yanga B kuingia fainali ya kombe la Uhai mwaka huu!

Sina mengo jamani tuonane tena wiki ijayo

Mwandishi wa makala hii ni mchambuzi wa michezo na burudani hapa nchini na anapatikana kwa namba 0652 626627.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI