MAKALA: MGOGORO SIMBA UMEPANDIKIZWA.

Na Prince Hoza

KWA sasa hawakai kiti kimoja, wamegombana, ni mgogoro mkubwa unafukuta katika klabu ya Simba unaowahusisha viongozi wa juu wa timu hiyo, mgogoro huo umesababisha kutimuliwa kwa makocha Abdallah Kibadeni na msaidizi wake Jamhuri Kihwelo 'Julio'.

Pia umesababisha kuajiliwa kocha mpya Zdravkos Lugarusic, pia umesababisha wapenzi na wanachama wa timu hiyo kugawanyika, katika sehemu ya mgogoro wa klabu ya Simba chanzo inasemekana ni mwenyekiti wao Ismail Aden Rage.

Baadhi ya viongozi wa klabu hiyo kongwe Afrika mashariki na kati kupitia kamati ya utendaji waliitisha mkutano kwa lengo la kumjadili mwenyekiti wao ambaye alikuwa safarini nje ya nchi kikazi, katika mkutano huo waliamua kumsimamisha mpaka mkutano mkuu wa wanachama utakapoamua hatma yake.

Ndipo ulipoibuka mgogoro mkubwa uliopelekea mwenyekiti wa klabu hiyo aliyesimamishwa kupinga uamuzi wa kamati kumsimamisha na kuwasilisha malalamiko yake TFF, Lakini kamati ya utendaji ya klabu hiyo iliendelea na msimamo wake ambapo sasa ilimpandisha chezo aliyekuwa kaimu makamu mwenyekiti Joseph Itang'are maarufu Kinesi kuwa kaimu mwenyekiti.


Uamuzi huo uliendelea kupingwa na Rage pale alipoitisha mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika makao makuu ya klabu hiyo mtaa wa Msimbazi, Hali si shwari ndani ya klabu hiyo, Rage alipinga maamuzi ya kumleta kocha mpya Mcroatia Lugarusic huku akitaka Kibadeni na Julio waendelee na kazi.

Kamati ya utendaji inayosikilizwa zaidi na wengi likiwemo shirikisho la soka nchini TFF, iliamua kumleta kocha huyo mpya aliyewahi kuinoa Gor Mahia ya Kenya, kwa sasa unaweza Rage hayupo Simba, amekubali kusimamishwa kwake na anasubiri mkutano mkuu umaue hatma yake.

Lakini shirikisho la kandanda nchini TFF kupitia rais wake Jamal Malinzi ilimpa Rage siku 14 kuitisha mkutano wa dharula wa pande zote ili kuweza kutuliza mgogoro huo, Rage alikataa agizo hilo la TFF kwa madai TFF haina mamlaka ya kuingilia katiba ya Simba.

Lakini TFF ilisema endapo Rage atakataa agizo la kuitisha kikao watampa adhabu kali, siku 14 za Rage zimekwisha kilichobaki sasa tunasubiri maamuzi ya TFF, kamati ya utendaji ya Simba nayo inasubiri maamuzi ya TFF ili iendelee na kazi yake.

Kwanza naisifu kamati ya utendaji kwa kazi yake kwani hadi sasa Simba imekaa pazuri, imeanza mazoezi chini ya kocha mpya na imeendelea kufanya usajili wake tena kwa kishindo, Simba imemsajili Awadh Juma toka Mtibwa Sugar, Badru Ally wa Suez Canal ya Misri, Yaw Berko mchezaji huru pamoja na kumchukua kocha wa zamani wa Gor Mahia.

Aidha Simba iko mbioni kumalizana na kipa wa zamani wa Yanga Ivo Mapunda ambaye anaichezea Gor Mahia ya Kenya, Kuna tuhuma mbalimbali zilitolewa mara baada ya uamuzi wa kumsimamisha Rage kuiongoza Simba.

Tuhuma hizo zinazomlenga ni zile za kuigeuza Simba kama taasisi yake binafsi, Rage amekuwa akifanya maamuzi mbalimbali nyumbani kwake huku akitangaza adhabu na uteuzi bila kutumia katiba, hivi karibuni Rage alimteua Michael Richard Wambura kuwa mjumbe wa kamati ya utendaji kinyume na taratibu.

Rage amehusika kuibomoa klabu ya Simba baada ya kuwauza Emmanuel Okwi, Mbwana Samatta, Patrick Ochan, Mwinyi Kazimoto na Shomari Kapombe huku fedha zikishindwa kuonekana, pia alitoa ahadi ya uongo pale alipowahadaa wanachama wa klabu hiyo wakati akitetea usajili wa Kelvin Yondani na Mbuyu Twite.

Rage aliwaambia wanasimba kuwa Yondani na Twite ni mali ya Simba na kama wakiichezea Yanga yeye atajiuzulu, lakini mabeki hao mahiri wameitumikia Yanga msimu uliopita na kuipa ubingwa wa bara, pia kamati hiyo iliona kuwa Rage anamapungufu mengi baada ya kuisigiza katiba ya Simba.

Hivyo hawakuona umuhimu wa kuendelea kuiongoza Simba na kuamua kumsimamisha uenyekiti, hapo ndipo mgogoro ulipoibuka upya na sasa kama umewaka moto, licha ya ukimya wake uliopitiliza Rage bado ajatangaza kujiuzuru wala kusema kuwa amekubali maamuzi ya kamati ya utendaji.

Amebakia kimya muda wote, waswahili husema kimya kingi mshindo mkubwa!  kukaa kwake kimya kunaweza kusababisha mpasuko mwingine mkubwa pindi akiibuka, Simba inajiandaa na mchezo wa ngao ya hisani dhidi ya hasimu wake Yanga utakaopigwa kwenye uwanja wa Taifa Desemba 21 mwaka huu mchezo unaojulikana kama MTANI JEMBE.

Lakini mimi naona kama mgogoro huo umepandikizwa na watu fulani wasioutakia mema uongozi wa Ismail Rage,  kwanini nasema hivyo kwa sababu Rage ndiye mwenyekiti halali wa Simba, TFF wakati inafanyia marekebisho ya katiba yake iliamua kuweka kipengere kipya cha kuwalinda viongozi halali wa vilabu.

Kumekuwa na tabia ya kuwang'oa viongozi madarakani mara tu timu inapofanya vibaya, yamekuwa maslahi ya mtu binafsi anapoona fulani hamtaki basi anapitisha kampeni ya chini kwa chini kumtoa, TFF iliona umuhimu na kuweka msimamo mkali dhidi ya Wanamapnduzi.

Yanayofanyika Simba ni kama mapinduzi, kama kuna watu hawamtaki Rage basi wasubirie muda wake utakapokwisha na ndio wamuweke wamtakaye, kuna kundi la wanachama na mashabiki wa Simba wanataka kuelekea kwa spika wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe Anne Makinda mjini Dodoma.

Lengo la safari hiyo ni kushinikiza Rage ajiuzuru bila ya ridhaa yake, Nikiwa kama mpenda michezo nchini hasa soka, nawaomba wanamichezo wenzangu hasa wale wanasimba kuachana na dhana hii potofu ya kutaka Rage aondolewe katika nyadhifa yake.

Wasubirie kipindi chake cha uongozi kikome ili haki na demokrasia ifanye kazi yake na kumchagua kiongozi mwingine mwenye mapenzi mema ya kuiongoza Simba, hakuna aliyevunja katiba kati ya Rage na kamati yake, kama kuivunja wote wamevunja, na kama kuisigiza wote wameisigiza.]

Haiwezekani mwqenyekiti asafiri ndio muitishe kikao, ridhaa ya kuitisha kikao amewapa nani! tuache kuongoza kwa visasi kama alivyosema rais wetu Jakaya Kikwete alipohutubia jana kwenye kilele cha sherehe za Uhuru wa Tanzania bara kwenye uwanja wa Uhuru.

Kikwete alisema kuwa tuige nyayo za mzee Nelson Mandela rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini ambaye hakupenda siasa za kulipa kisasi pindi alipoachiwa kutoka jela ambapo alifungwa na makaburu wakati akitetea haki za watu weusi waliokuwa wakiteswa na kuuawa na makaburu walioendeleza siasa za ubaguzi wa rangi.

Kwa leo naishi hapo tuonane mwishoni mwa wiki ambapo nitawaletea makala nyingine ya uchambuzi, Mwandishi wa makala hii anapatikana kwa namba 0652 626627, Toa maoni yako.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA