KUNANI YANGA! NGASA, MSUVA WATIMKA.

Yanga imepata pigo baada ya winga wake, Mrisho Ngasa, Simon Msuva na beki wa kati Nadir Haroub 'Cannavaro' kuugua jambo litakalowafanya kuwa nje ya uwanja kwa siku kadhaa, hivyo kuzikosa mechi za mwanzo za michuano ya Kombe la Mapinduzi inayoanza kesho visiwani Zanzibar.

Katika ratiba iliyotolewa na waandaaji wa michuano hiyo, inaonyesha Yanga itaanza kwa kucheza dhidi ya Tusker ya Kenya keshokutwa.
Ngasa anasumbuliwa na homa ya matumbo wakati Cannavaro ni majeruhi wa goti huku Simon Msuva akisumbuliwa na malaria.

Hali hiyo ilimfanya Ngasa kuyakosa mazoezi ya Yanga yaliyofanyika kwa saa mbili jana kuanzia saa 3:00 - 5:00 asubuhi chini ya Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Felix Minziro. Wachezaji wengine ambao hawakuwapo jana ni pamoja na washambuliaji Waganda, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza, winga Msuva na kiungo Salum Tetela.


Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Daktari wa Yanga, Nassoro Matuzya, alisema Ngasa anasumbuliwa na maradhi ya tumbo na atakuwa nje ya uwanja kwa takriban wiki nzima ili kukamilisha dozi ya dawa aliyoianza juzi.

"Ngasa alipimwa jana (juzi) na kugundulika kusumbuliwa na maradhi ya tumbo. Ameanza kumeza dawa ambazo dozi yake itakamilika ndani ya siku tano. Baada ya hapo tutaangalia kama kutakuwa na uwezekano kuungana na wachezaji wenzake katika timu," alisema Matuzya.

"Msuva naye hajisikii vizuri leo (jana) na mchana huu atafanyiwa vipimo vya afya kwenye Hospitali ya Mwananyamala. Telela na Cannavaro (Nadir Haroub) nao hawako vizuri na wako nje ya kikosi. Telela ni majeruhi kwa muda mrefu na atarejea uwanjani Ijumaa. Cannavaro anasumbuliwa na jeraha la goti," alifafanua zaidi daktari huyo.

Yanga, ambao wanasaka kocha mpya baada ya kutangaza kuachana na Mholanzi Ernie Brandts aliyewapa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu uliopita, wamepangwa Kundi C katika Kombe la Mapinduzi, michuano itakayoshirikisha timu 12, pamoja na mabingwa watetezi, Azam FC, Tusker ya Kenya na Unguja Combine.

Kundi A kuna Mbeya City, Pemba Combine, Chuoni na URA kutoka Uganda wakati Kundi B lina timu za Simba, KMKM, AFC Leopards ya Kenya na KCC ya Uganda.

Pazia la mashindano hayo litafunguliwa kesho kwa mechi mbili za Kundi B kwenye Uwanja wa Amaan, saa 10:00 alasiri kwa mabaharia wa KMKM kupambana na Manispaa ya jiji la Kampala (KCC).

Aidha, saa 2:00 usiku, 'Wekundu wa Msimbazi', Simba, watakuwa kibaruani dhidi ya AFC Leopards.

Keshokutwa kutakuwa na mechi nne kwenye viwanja vyote viwili vya Amaan, Unguja na Gombani, Pemba. Uwanja wa Amaan kutakuwa na mchezo kati ya mabingwa watetezi Azam FC dhidi ya Unguja Combine kuanzia saa 10:00 alasiri na Yanga dhidi ya Tusker itakayorindima kuanzia saa 2:00 usiku.

Uwanja wa Gombani shughuli itakuwa kati ya URA na Chuoni (Kundi C) watakaovaana saa 8:00 mchana huku Mbeya City ikitoana jasho na Pemba Combine kuanzia saa 10:00 jioni katika mchezo wa Kundi A.

Fainali ya michuano hiyo itapigwa Uwanja wa Amaan Januari 12 kuanzia saa 2:00 usiku, siku ambayo ndiyo kilele cha maadhimisho ya sherehe za miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Wakati huo huo, Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh, alisema hadi jana mchana walikuwa hawajafahamu wataondoka lini kuelekea Zanzibar licha ya kufahamu mechi yao ya kwanza itachezwa keshokutwa.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA