IVO MAPUNDA ASAINI SIMBA MIAKA MIWILI.
Uongozi wa Simba umesema upo katika hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kipa mkali wa kupangua mikwaju ya penalti Mtanzania Ivo Mapunda.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspope alisema uongozi wa 'Wanamsimbazi' hao
umekubaliana kumpa mkataba wa miaka miwili kipa huyo wa zamani wa watani wao wa jadi, Yanga.
"Kwa sasa tunamsikiliza kocha (Mcroatia Zdravok Logarusic) kama kuna mchezaji mwingine anayemhitaji baada ya kumpata Ivo.
Tumekubaliana tumpe mkatana wa miaka miwili ambao atausaini mara tu baada ya mashindano ya Kombe la Chalenji," alisema Hanspope.
Alisema wametenga fungu nono ambalo limemshawishi nyota huyo kujiunga nao.
Hata hivyo, Hanspope hakuwa tayari kuweka wazi kiasi cha fedha za usajili na mshahara ambao Ivo atakuwa akilamba katika klabu hiyo ambayo kwa sasa inakabiliwa na mgogoro wa uongozi.
Simba imeonekana kutoridhishwa na kiwango cha kipa wake Mganda, Abel Dhaira baada ya kuamua kumsajili kwa muda wa miezi sita kipa wa zamani wa Yanga, Mgana Yaw Berko na sasa inamalizia usajili wa kipa mzawa Ivo.
Kipa huyo aliyeipa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya klabu yake ya sasa ya Gor Mahia msimu uliopita na kujizolea umaarufu wa kupangua michomo ya penalti nchini humo, Jumamosi alidaka penalti mbili kati ya tatu walizokosa Uganda na kuiwezesha Timu ya Taifa ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars) kutinga hatua ya nusu fainali ya mashindano ya Kombe la Chalenji.
Mashindano hayo yalianza Novemba 27 na yatafikia tamati Desemba 12, mwaka huu yakishirikisha timu za taifa za nchi 11 za Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati huku mabingwa wa zamani wa Afrika, Zambia wakishiriki kama timu alikwa.
Kanuni mpya ya Shirikisho la Soka nchini (TFF) inayozitaka timu kuwa na wachezaji wa kigeni wasiozidi watatu na makipa wazawa kuanzia msimu ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, huenda ikailazimu Simba kuachana na Dhaira na Berko na kubaki na Ivo na makipa wengine wazawa ili kukidhi matakwa ya Azimio la Bagamoyo.