YANGA WAITANGAZIA KIAMA SIMBA JUMAPILI

Mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga wamesema wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya watani wao wa jadi, Simba katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara utakaopigwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.


Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Utendaji, Baraza la Wazee na matawi ya Yanga ya jiji la Dar es Salaam kilichofanyika kwenye ofisi za makao makuu ya klabu hiyo jijini jana, msemaji wa matawi hayo, Bakili Makele alisema mipango ya 'kumuua mnyama' imeshakamilika na wameshahakikishiwa kuibuka na ushindi wa magoli 3-0 katika mchezo huo mgumu dhidi ya vinara wa ligi.

"Leo (jana) tumekutana matawi yote ya Yanga ya Dar es Salaam, Baraza la Wazee na Kamati ya Utendaji kujadili namna ya kumuua Mnyama.

Tumepokea taarifa kutoka kwenye Kamati ya Utendaji, Sekretarieti na Baraza la Wazee la Yanga kwamba mipango yote inakwenda vizuri, hakuna matatizo kwenye timu na hatuna majeruhi hata mmoja. Tunapiga magoli matatu Jumapili," alisema Makele.

"Tunaomba nidhamu kwa wanachama na mashabiki wa Yanga siku hiyo. Tunaomba pia refa na wasaidizi wake siku hiyo wawe makini maana wapinzani wetu mechi zao ni za penalti. Kila mechi wachezaji wao wanajiangusha na kupewa penalti zisizo halali," alisema zaidi Makele, ambaye pia ni kiongozi wa Tawi la Yanga la Temeke.

Naye Katibu wa Baraza la Wazee la Yanga, Ibrahim Akilimali aliahidi ushindi mnono siku ya Jumapili katika mchezo huo na kubainisha kuwa viongozi, makocha na wachezaji wameshamaliza kazi na kilichopo kwa sasa wao wanamalizia kazi ili kunogesha ushindi huo.

"Yanga tuna tamaduni zetu, sehemu yoyote ile ina asili yake, hivyo kwa hivi sasa sisi wazee kwa pamoja tunaahidi lazima tumchinje mnyama Jumapili. Uwezo na nia tunayo, hivyo washabiki wa Yanga mje kwa wingi Uwanja wa Taifa kuishangilia timu yetu" alisema Akilimali.

"Baada ya kufungwa 3-2 na Azam, nilisema kwamba Yanga sasa inaanza ligi. Watani wetu wanaweweseka kuona 'speed' (kasi) yetu ni ya hali ya juu, tunachoomba ni waamuzi kuchezesha soka kwa kufuata kanuni 17 za mchezo. Yanga si timu ya kuhurumiwa na marefa, na kama watafuata sheria 17 za soka, basi lazima tumchape mnyama.

"Watani wetu walitufunga 5-0, sisi (Yanga) hatutawafunga magoli hayo katika mchezo mmoja bali tutajibu kwa kushinda michezo mitano mfululizo dhidi ya Simba. Hapo tutaona nani atakayeumia zaidi; aliyefungwa 5-0 katika mchezo mmoja au aliyepoteza michezo mitano mfululizo," aliongeza Akilimali.

Ofisa Habari wa Yanga, Baraka Kizuguto alisema jana kuwa kikosi chao kinaendelea vizuri na mazoezi kisiwani Pemba kujiandaa kwa mchezo huo utakaochezeshwa na refa mwenye beji ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA) Israel Nkongo wa Dar es Salaam, ambaye aliwahi kukunjwa na kupigwa na baadhi ya wachezaji wa Yanga katika mchezo wa ligi hiyo waliyolala 3-1 dhidi ya Azam FC msimu wa 2011/12.

Meneja wa Yanga, Hafidh Saleh aliiambia NIPASHE akiwa Pemba baada ya mazoezi ya jana kuwa wachezaji wote 29 walioidhinishwa kuitumikia Yanga msimu huu wako 'fiti' kwa ajili ya mchezo huo utakaokuwa wa tatu (wa watani) kwa kocha Mholanzi Ernie Brandts tangu atue Septemba mwaka jana kuchukua mikoba ya kocha Mbelgiji Tom Saintfiet aliyetimuliwa.

Mholanzi huyo aliyetua Yanga akitokea klabu ya 'maafande' wa APR ya Rwanda aliyoifundisha tangu 2010, aliiongoza Yanga kuichapa Simba 2-0 katika mchezo wao wa mwisho wa kufunga msimu uliopita wa Ligi Kuu ya Vadacom Tanzanbia Bara iliyochezwa Mei 18 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Taarifa zilizotufikia jana kutoka ndani ya uongozi wa Yanga zilieleza kuwa kikosi chao kitaingia Dar es Salaam muda wowote kuanzia leo jioni kikitokea Pemba tayari kwa mchezo wa keshokutwa.

"Timu itatua Dar es Salaam kwa ndege muda wowote kuanzia kesho (leo) jioni na itafikia kwenye moja ya hoteli nzuri za jiji hili kuendelea na kambi," alisema mmoja wa 'vigogo' wa Yanga ambaye aliomba jina lake lisitiriwe.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA