PINDA AMWEKA MATATANI MAGUFULI

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ametengua maamuzi yaliyofanywa na Waziri wa Ujenzi Dk. John Magufuli ya kuongeza tozo ya asilimia tano kwa wasafirishaji wa malori na mabasi kwa uzito unaozidi.


Agizo la kurudisha asilimia hiyo ya tozo ilitangazwa na Dk. Magufuri Oktoba Mosi mwaka huu na kusababisha manung’uniko kutoka kwa wasafirishaji huku wa malori wakigoma kuanzia juzi.

Waziri Mkuu aliitangaza uamuzi huo jana jijini Dar es Salaam mbele ya waandishi wa habari.

Pinda alisema baada ya kukutana na wadau wa usafirishaji nchini na kusikiliza maelezo yao, alibaini masuala kadhaa ambayo aliona ni vyema yakaangaliwa upya ili sekta hiyo isizorote na baada ya hapo alikutana na Baraza la Mawaziri na kukubaliana mambo kadhaa.

“Kwa kuwa kuna mvutano kati ya Wizara ya Ujenzi na wasafirishaji wa malori na mabasi kuhusu kanuni ya 7 (3) ya Sheria ya Usafirishaji ya mwaka 1973,  kwamba haitekelezeki kirahisi,  nimeiagiza  wizara  ikutane na wadau mbalimbali kwa ajili ya kupitia kila jambo linalohitajika,” alisema.

Wadau hao ni Wizara ya Ujenzi, Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Viwanda na Biashara, Chama Cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), Chama cha Wamiliki wa Malori (Tatoa), Ofisi ya Waziri Mkuu  na ya  Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Pinda alisema: “Tumewapa mwezi mmoja wa kulishughulikia suala hili kwani ni jambo linalohitaji uamuzi mzuri, na tunategemea kuwa watakuja na majibu mazuri kwa muda tuliowapa.”

Aliongeza: “Nalisema hili kwa kuwa sisi kama nchi tunapaswa kuliangalia vizuri, na ni lazima tuziangalie barabara zetu tunazozijenga kwa gharama kubwa.”

Pinda alisema kutakuwa na uwezekano wa kuwapo kwa msongamano wa mabasi na malori kwenye mizani na serikali imeshauri kuwa mizani ya Kibaha itumike kwa ajili ya mabasi tu na ile ya Mikese kwa ajili ya malori, na kwamba  njia za Tanga, Moshi na Arusha zitalazimika kutafutiwa utaratibu mwingine wa mizani.

Pia aliitaka timu hiyo, wakati wa majadiliano yao, kuangalia suala la watumishi ambao siyo waaminifu kwenye mizani.

“Wakati naongea na wadau hao mmoja aliniambia kuwa bado kuna matatizo kwenye mizani kwani alisema gari lake lilizuiliwa kwa kuwa lilipatikana na kosa, lakini  alitoa rushwa na akaachiwa, kwa hiyo tatizo hilo bado lipo na linapaswa kuangaliwa,” alisisitiza.

Alisema jambo jingine linalopaswa kuangaliwa ni hali ya mizani, kwani kuna malalamiko kuhusu utofauti wa uzito katika baadhi ya mizani na kwamba amehakikishiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kwamba wapo mbioni kufunga mizani nyingine ambazo ni za kisasa zaidi.

Pia alitaka kuwapo kwa mawasiliano kati ya taasisi za serikali hasa pale linapotokea jambo linaloigusa sekta nyingine ili wapate kuzungumza  na kwamba katika hali ya sasa ni vyema ukawapo utaratibu wa kuwashirikisha wadau katika kila sekta hizo ili kuleta uelewano.

Kuhusu chimbuko la mgogoro, Pinda alisema kulikuwa na mambo mawili, ambayo ni barua ya aliyekuwa Waziri wa Ujenzi wa wakati huo, Basil Mramba, ambayo aliiandika mwaka 2006 ya kutoa msamaha kwa tozo kwa uzito wa magari uliozidi ndani ya asilimia tano ya uzito unaokubaliwa kisheria.

“2006 Mramba alipata taarifa kuwa mizani ina matatizo na akaona aweke utaratibu wa ahueni kidogo, kwa hiyo barua hiyo ikawa inatumika isivyo sawa kwani kila aliyezidisha uzito alitumia mwanya huo ili asilipishwe na hivyo kuchangia kutokuwapo kwa uadilifu,” alisema.

Alitaja jambo lingine kuwa ni la kisheria, na kwamba Waziri Magufuli aliamua kutumia sheria kwa kuwa mwongozo wa Mramba haukuwa wa kisheria pamoja na kwamba uamuzi wake ulikuwa na nia njema.

HALI SI SHWARI BANDARINI

Wakati huo huo, hali si shwari katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na eneo hilo kujaa mizigo bila kuondolewa ndani ya siku hizo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Mamlaka ya Usimamizi Bandari (TPA), Janeth Ruzangi, alisema hali ya bandari siyo shwari kwa kuwa nafasi haipo tena kwa ajili ya kuwekea mizigo na makontena vinavyoshushwa kutoka kwenye  meli zinazotia nanga katika bandari hiyo tangu mgomo huo uanze siku tano zilizopita.

Alisema kulikuwa na takribani tani 23, 165 za mbolea ambazo zilikuwa zimeshushwa bandari hapo na kwamba hadi jana mchana mizigo hiyo ilikuwa haijaondolewa kwa kuwa hakuna malori yaliyofika hapo kwa ajili ya kupakia na kisha kuondoka nayo.

Mtandao huu ulishuhudia kuwapo kwa mizigo hiyo ya mbolea aina ya urea ikiwa imepangwa katika maeneo mbalimbali na kuonekana kuchukua nafasi kubwa kwenye eneo hilo.

Sambamba na hilo, takribani meli tisa za mizigo ya kawaida zilitakiwa kubaki baharini bila kushusha shehena kwa vile hakuna nafasi ya kuweka wala malori ya kupakia.

Ruzangi alisema meli mbili ni za ngano, nne za magari, moja ya mbolea, mbili za vyuma huku eneo la upakuaji likiwa na meli tatu.

Naye Kaimu Meneja, Kitengo cha  Mafuta bandarini, Abdul Mwingamno, alisema athari ya mgomo huo haijagusa kitengo chake kwa kuwa meli za mizigo hiyo zikiingia zinaenda moja kwa moja kwenye eneo la matanki na hivyo kutoathiri nafasi.

 TPA katika kufanikisha utendaji wa bandari hiyo inayotegemewa kwa kukuza uchumi wa taifa, imeanzisha mradi wa boya jipya linalojulikana kama Single Point Mooring (SPM), ambalo kwa mujibu wa Ruzangi, limepunguza siku za meli kukaa bandarini kutoka 45 hadi moja tangu lianze kufanya kazi Novemba 15 mwaka jana.

TATOA YAZUNGUMZA

Baada ya uamuzi wa Pinda, mjumbe wa Bodi ya Tatoa, Zacharia Hanspoppe, alisema wamesikia maamuzi hayo, lakini nao wataenda kama bodi na kutoa msimamo wao rasmi juu ya kauli hiyo.

“Siwezi kuongea mengi kwa kuwa mimi si msemaji, ila yote yataamuliwa kwenye kikao cha bodi leo jioni (jana),” alisema.

Kwa upande wao, kampuni ya Consolidated Transporters, mwanachama wa Tatoa, katika barua yao iliyotumwa kwa vyombo vya  habari, ilimwomba Rais Kikwete na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinuduzi ya Zanzibar, Dk. Alli Mohammed Shein kuliangalia kwa makini suala hilo ikiwa ni pamoja na kifungu hicho cha sheria na namna Waziri Magufuli alivyotumia maamuzi yake mwenyewe.

TABOA WAMPONGEZA  PINDA

Katibu Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi nchini (Taboa), Enea Mrutu, alisema kuwa, kama chama wanashukuru kauli ya Waziri Mkuu kwa kuwa amesikia kilio chao lakini wanatarajia kukutana naye ili kujadili zaidi kuhusu tatizo la mizani.

Imeandikwa na Isaya Kisimbilu, Samson Fridolin na Enless Mbegalo, Dar.
Mwisho.

BARAZA la Watumiaji wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra CCC), limelaani mgomo wa mabasi ulioitishwa Oktoba 8 mwa ka huu   na Chama Cha Wamiliki wa Mabasi nchini Taboa.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana  Mwenyekiti wa Baraza hilo Ayoob Omari alisema kuwa kitendo kilichofanywa na Chama hicho kwa kuwa kilikiuka haki za msingi za watumiaji wa huduma za usafiri wa Barabara hususani haki ya kupewa taarifa , pamoja na haki ya usalama wao bila sababu ya msingi.

Omari aliongeza kuwa Baraza lake linawataka abiria wote walioathiriwa na mgomo huo kuwasilisha malalamiko yao kwenye makampuni waliyokuwa wasafiri nayo, na kupeleka nakala ya madai hayo kwa ajili ya kudai fidia kutokana na usumbufu uliojitokeza.

Omari aliwakumbusha wamiliki wa mabasi kuwa abiria akishakata tiketi anakuwa ameingia kwenye mkataba na kampuni zao na kitendo cha kugoma kwa sababu ambazo hazina uhusiano wa moja kwa moja na abiria hakina uhalali wowote wa kukatisha mkataba na abiria.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA