NGASA, KIIZA WAUNDA BENDI YAO............

Winga  hatari wa Yanga na timu ya Taifa (Taifa Stars), Mrisho Ngasa amesema ushirikiano mzuri wanaouonyesha wakicheza sambamba na Mganda Hamisi Kiiza, umewafanya waunde bendi  yao ya uwanjani inayokwenda kwa jina la 'Danger Zone'.

Ngasa ambaye ameifungia Yanga mabao matatu katika mechi tano alizocheza msimu huu tangu atoke kifungoni huku akitoa pasi tano za mwisho, anaamini kujituma kwake mazoezini na kwenye mechi ndiko kunakomfanya ang'are katika kikosi cha klabu yake msimu huu wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.


Akizungumza baada ya kumalizika kwa mechi ya juzi waliyoshinda 3-0 dhidi ya Rhino Rangers kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Ngasa alisema kucheza kwa kujituma na kushirikiana vizuri na wachezaji wenzake, kumemsaidia kutisha katika Kikosi cha Yanga.

"Namshukuru Mungu kwa kunisaidia kufanya vizuri licha ya kuandamwa na jambo zito la kusimamishwa kucheza mwanzoni mwa ligi na kulipa mamilioni ya shilingi.

Nafanya mazoezi kwa nguvu na kujituma sana, pia nikiwa kwenye mechi nashirikiana na wachezaji wenzangu," alisema Ngasa.

"Kwa sasa tuna 'kombinesheni' (muunganiko) kali kwenye safu yetu ya ushambuliaji ambayo tumeamua kuiita Bendi ya 'Danger Zone' kwa sababu mimi na Kiiza tunapokuwa kwenye eneo la hatari muda wowote tunafanya maajabu," alifafanua Ngasa.

Winga huyo alifungiwa mechi sita na Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka nchini(TFF), tano za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara na mechi moja ya Ngao ya Jamii waliyoshinda 1-0 dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa Taifa Agosti 17, mwaka huu baada ya kubainika kuwa alisaini mikataba ya kuzitumikia klabu mbili, Simba na Yanga msimu huu.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA