KUMUONA TAMBWE, KAVUMBAGU 5000 TAIFA......

Kiingilio cha chini cha mechi ya watani wa jadi, Simba na Yanga itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kitakuwa ni Sh.5,000 kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Shirikisho la Soka (TFF).


Taarifa hiyo iliyosainiwa na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura ilieleza pia kwamba mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara itachezeshwa na refa mwenye beji ya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA), Israel Nkongo.

Ilieleza kuwa kiingilio hicho cha chini kitakuwa ni kwa viti vya rangi ya kijani ambavyo ni 19,648.

Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu kiingilio ni Sh. 7,000, viti vya rangi ya chungwa itakuwa Sh. 10,000, VIP C kiingilio ni Sh. 15,000, VIP B itakuwa Sh. 20,000 wakati VIP A yenye viti 748 tu tiketi moja itapatikana kwa Sh. 30,000.

Wambura alisema kuwa tiketi zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo huo utakaoanza saa 10 kamili jioni katika vituo mbalimbali.

Alivitaja vituo hivyo kuwa ni Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala, Uwanja wa Uhuru, na BMM Salon iliyoko Sinza Madukani.

Katika mechi hiyo namba 63, refa Nkongo kutoka Dar es Salaam atasaidiwa na Hamis Chang'walu wa Dar es Salaam pia, na Ferdinand Chacha wa Kagera. Mwamuzi wa akiba ni Oden Mbaga wa Dar es Salaam ambaye pia ana beji ya FIFA.

Kamishna wa mechi hiyo atakuwa John Kiteve kutoka Iringa wakati mtathmini wa waamuzi (referees assessor) ni Stanley Lugenge wa Njombe.

Timu ya Yanga iko kambini Pemba kwa ajili ya kujiandaa na mechi hiyo wakati Simba iko Bagamoyo mkoani Pwani.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI