HAIJAPATA KUTOKEA BARANI AFRIKA...............

Furaha ya kupita kiasi ndiyo iliyosababisha zaidi ya watu 20 kuzimia uwanjani wakati walipokuwa wakishuhudia mchezo wa Ligi Kuu kati ya Simba na Yanga uliofanyika juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Katika mchezo huo uliokuwa umejaa na presha kubwa kuanzia kwa wachezaji hadi kwa mashabiki wa pande zote mbili ulimalizika kwa timu hizo kufungana mabao 3-3.


Kwa mujibu wa Kiongozi wa Kikosi cha Maafa cha Msalaba Mwekundu, Bushiri Mgamba aliyekuwa akiongoza kikosi cha huduma ya kwanza uwanjani hapo alisema kuwa sababu kubwa ya watu hao kuzimia ilitokana na kuwa na furaha kupita kiasi.

Alisema baadhi ya watu wanapokuwa na furaha kupita kiasi wanapatwa na hali hiyo, lakini siyo kwa kila mtu na ndiyo maana hiyo juzi waliozimia uwanjani hapo walikuwa wachache ingawa waliokuwa na furaha walikuwa ni wengi.

“Hali hiyo pia inaweza kuzuilika, ambapo ni mtu mwenyewe anaweza kujizuia ili isimpate,” alisema Mgamba.

Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa kikosi hicho cha maafa cha Msalaba Mwekundu ambaye pia aliwahi kuwa daktari wa timu ya Yanga, Juma Sufiani aliliambia gazeti hili kuwa katika mechi hiyo watu wengi walizimia kipindi cha kwanza.

Alisema watu hao walipatwa na hali hiyo baada ya Yanga kufunga bao la pili na lile la tatu, mabao ambayo yalipachikwa wavuni na Hamis Kiiza.

“Mabao hayo yalisababisha watu hao kuzimia ambao wengi wao walikuwa ni mashabiki wa Yanga kwani walikuwa na furaha kupita kiasi na kujikuta wakizimia.

“Pia katika kipindi cha pili cha mchezo huo hali hiyo ilihamia upande wa mashabiki wa Simba, ambapo napo baadhi yao walizimia, ilikuwa ni baada ya timu hiyo kupata bao la pili na la tatu yaliyofungwa na Joseph Owino na Gilbert Kaze,” alisema Sufiani.

Aliongeza kuwa, ‘‘Watu hao walipatiwa huduma uwanjani hapo na hali zao ziliendelea vizuri na hadi kufikia jana kulikuwa hakuna taarifa yoyote mbaya.”

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Angetile Osiah aliliambia gazeti hili kuwa hali hiyo ilikuwa ni ya kushangaza, lakini walikuwa wamejipanga vilivyo kukabiliana na tukio lolote ambalo lingetokea uwanjani hapo.

“Tulikuwa tumejipanga vizuri kabisa, watu wa huduma ya kwanza walikuwapo wa kutosha na wote waliopatwa na hali hiyo walipatiwa huduma, ni matumaini yetu kuwa hali zao ni nzuri kwani hadi sasa hatuna taarifa yoyote mbaya,” alisema Osiah.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA