BARTHEZ AREJESHWA YANGA........

Benchi la ufundi la Yanga limemsafisha kipa wake namba moja, Ally Mustapha ‘Barthez’ dhidi ya shutuma anazotupiwa na mashabiki wa timu hiyo tangu siku ya Jumapili baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Simba.

Mashabiki hao wanamshutumu Barthez kuwa alichangia timu hiyo ishindwe kuibuka na ushindi katika mchezo huo uliomalizika kwa sare ya bao 3-3 ikiwa ni baada ya Yanga iliyokuwa ikiongoza kwa mabao 3-0 katika kipindi cha kwanza kuruhusu wapinzani wao hao wa jadi Simba kusawazisha mabao yote kipindi cha pili cha mchezo huo.


Hali hiyo iliwafanya mashabiki hao kuanza kumshutumu Barthez kuwa ndiye aliyeihujumu timu yao katika mchezo huo ambao ulikuwa na ushindani mkubwa.

Kocha msaidizi wa Yanga, Felix Minziro amesema kuwa wanaomshutumu kipa huyo hawajui mpira kwani hali iliyotokea katika mechi hiyo ni ya kimchezo ambayo inaweza kutokea kwa timu yoyote ile.

Alisema shutuma hizo anazotupiwa Barthez na baadhi ya mashabiki wa timu hizo hazina ukweli wowote isipokuwa zimelenga kumchafua, lakini wao kama benchi la ufundi la timu hiyo bado wana imani naye na wataendelea kumwamini kama walivyokuwa wakimwamini hapo awali.

“Matokeo kama hayo siyo ya kwanza kutokea kwa Yanga, timu inaweza kuongoza kwa muda mwingi, lakini dakika chache tu kabla ya kumalizika kwa mchezo matokeo yakabadilika.

“Hivyo mashabiki wetu wanapaswa kulijua hilo na tunawaomba waendelee kumuunga mkono Barthez, pia wanatakiwa kutambua kuwa  maotokeo ya Jumapili dhidi ya Simba ni ya kawaida katika soka,” alisema Minziro.

Aliongeza kuwa,”Kutoonekana kwa Barthez katika mechi yetu dhidi ya Rhino Rangers jana (juzi) ni maamuzi ya benchi la ufundi,” alisema Minziro.

Katika hatua nyingine Minziro aliongeza kuwa timu hiyo itaendelea na mazoezi yake leo kwa ajili ya kujiandaa na mechi zake za Ligi Kuu zilizobakia

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA