YANGA YAANGUSHIWA KIPIGO CHA SHARUBELA
Matokeo hayo yaliwaacha Yanga wakiwa na pointi 6 baada ya mechi tano, wakitoka sare tatu mfululizo kabla ya kipigo cha jana.
Yanga ambao walianza ligi kwa kishindo wakiikaribisha timu iliyopanda daraja ya Ashanti United kwa magoli 5-1 katika mechi ya ufunguzi wa ligi, jana walitanguliwa kwa goli la sekunde ya 27 tu tangu mechi kuanza lililofungwa na mshambuliaji mrefu John Bocco 'Adebayor'.
Bocco alifunga goli hilo akimalizia kwa kichwa mpira uliobabatizwa na beki Kelvin Yondani wa Yanga aliyekuwa akiokoa mpira wa kichwa cha Brian Umony aliyepokea krosi murua ya winga aliyepandishwa timu ya wakubwa kutoka kikosi cha vijana cha Azam, Farid Musa na kufanya goli la mapema zaidi kufungwa kwenye ligi kuu ya Bara msimu huu.
Baada ya goli hilo kufungwa, Yanga walianza kulisakama kama nyuki lango la Azam huku wakitawala kipindi chote cha kwanza lakini umakini wa kipa Aishi Manula uliiokoa Azam kufungwa mvua ya magoli kwani alipangua mashuti matatu hatari yaliyolenga goli mashuti mawili ya Kavumbagu na Twite yakigonga mwamba.
Hadi mapumziko Azam walikuwa wanaongoza 1-0 huku Joackins Atudo akionyeshwa kadi ya njano na refa Dominic Nyamisana wa Dodoma kwa kupoteza muda
Dakika nne baada ya kuanza kwa kipindi cha pili, mshambuliaji Mrundi Didier Kavumbagu alisawazishia Yanga baada kukokota mpira kutoka katikati ya uwanja na kumlamba chenga kipa Manula kabla ya kuukwamisha mpira wavuni na kuwainua vitini mashabiki wa Yanga ambao walikuwa kimya.
Dakika ya 21 mtokeabenchi Hamis Kiiza, ambaye alikuwa ndiyo kwanza amerejea nchini akitokea kujaribu kucheza soka la kulipwa Uturuki, aliifungia Yanga goli la pili akimalizia kwa mguu wa kulia krosi kali ya Simon Msuva na kuifanya Yanga iwe mbele kwa magoli 2-1.
Azam walisawazisha goli hilo katika dakika ya 70 kupitia kwa mfungaji bora msimu uliopita, Kipre Tchetche, aliyefunga kwa penalti iliyoamuliwa na refa Dominic Nyamisana baada ya kiungo Haruna Niyonzima kushika mpira ndani ya boksi wakati akiokoa krosi ya Kipre Balou. Lilikuwa goli la kwanza kwa Tchetche tangu msimu huu uanze Agosti 24.
Joseph Kimwaga aliyeingia dakika ya 72 kuchukua nafasi ya Faridi Musa, aliifungia Azam goli la tatu na la ushindi baada ya wenyeji hao wa mechi ya jana kufanya shambulizi kali la kushtukiza katika dakika ya 90.
Goli hilo lilikuja sekunde chache tu baada ya Yanga kukosa goli la wazi. Mpira ulianza kwa kipa Manula kupangua kishujaa shuti kali la Simon Msuva kisha wakati Yanga wakionekana kujisahau mpira mrefu ukapigwa kwa winga huyo aliyepandishwa kutoka kikosi cha vijana cha Azam.
Akatulia na kumchambua vyema kipa Ali Mustapha 'Barthez' na kuipa timu yake ushindi wa pili katika mechi tano.
Jukwaa la Simba lililipuka kwa shangwe kufuatia kufungwa kwa goli la tatu ambalo lilishuhudiwa pia na benchi la ufundi la Simba lilikuwapo uwanjani likiongozwa na kocha msaidizi, Jamhuri Kihwelo 'Julio'.
Baada ya mechi hiyo kumalizika kocha wa Azam, Muingereza Stewart Hall alisema "timu bora imeshinda.
Yanga wamecheza vizuri lakini tumewazidi mbinu."
Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernie Brandts alisema: "Wachezaji wetu wamecheza vizuri, tumetengeneza nafasi nyingi lakini hatukuwa na bahati. Ligi ni ngumu,t utaendelea kujipanga zaidi."
Hiyo ilikuwa ni mechi ya kwanza kwa Yanga kupoteza msimu huu baada ya kutoka sare tatu mfululizo dhidi ya Coastal Union (nyumbani), Mbeya City na Prisons (ugenini).
Simba wanaendelea kuongoza ligi hiyo wakiwa na pointi 11 baada ya mechi tano.
Katika mechi nyingine za jana, JKT Ruvu walioanza ligi kwa kushinda mechi tatu mfululizo na kuongoza kwa muda msimamo wa ligi hiyo inayodhaminiwa na kampuni ya huduma za simu ya Vodacom Tanzania, jana walikumbana na kichapo cha pili mfululizo cha 1-0 dhidi ya wageni Oljoro JKT kwenye uwanja wa Mabatini, Pwani huku ndugu zao Ruvu Shooting wakipata kipigo kama hicho dhidi ya wenyeji Coastal Union kwenye uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Goli la Oljoro dhidi ya JKT Ruvu lilifungwa na Paul Malipesa katika dakika ya 79, wakati goli la Coastal dhidi ya Shooting lilifungwa na kiungo wa zamani wa Simba, Haruna Moshi 'Boban' katika dakika ya 80
Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa; Yanga: Ali Mustafa 'Barthez', Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Athuman Idd 'Chuji', Simon Msuva, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Jerson Tegete/ Hamis Kiiza (dk 60), Haruna Niyonzima.
Azam: Aishi Manula, Erasto Nyoni, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo/ Said Morad (dk 58), Himid Mao, Farid Musa/ Joseph Kimwaga (dk 72), Kipre Bolou, John Bocco 'Adebayor', Humphrey Mieno, Brian Umony/ Kipre Tchetche (dk 54).
TAKWIMU AZAM, YANGA
KONA: Azam 3, Yanga 3
MASHUTI: Azam 4 (Farid Musa dk 40, Kipre Balou 55, Joseph Kimwaga dk 82, 90), Yanga 11 (Kavumbagu dk 10, Twite dk 14 & 43, Msuva dk 27,49 na 89, Tegete dk 35 & 46, Domayo dk 63, David Luhende dk 80).
KUOTEA: Azam 5 (Bocco dk 27,42 & 77, Tchetche dk 76), Yanga 2 (Msuva dk 8, Tegete dk 53),
KADI YA NJANO: Kulikuwa kadi moja tu (ya njano) iliyotolewa kwa Atudo kwa kupoteza muda dk. 37
RAFU: Azam 8, Yanga 9
MABADILIKO: Azam 3, Yanga 1