TP MAZEMBE VITANI TENA OKTOBA 6

TOUT Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), itaanzia ugenini Nusu Fainali ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Stade Malien ya Mali, Oktoba 6, mwaka huu, kabla ya kurudiana wiki mbili baadaye mjini Lubumbashi.


Kwa mujibu wa Ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jana, mchezo wa kwanza utachezwa kwenye Uwanja wa Modibo Keita mjini Bamako kuanzia saa 10:00 jioni kwa saa za huko na saa 12:00 kwa saa za Afrika Mashariki.

Mechi hiyo itachezeshwa na refa Alioum Neant, atakayesaidiwa na Evarist Menkouande wote wa Cameroon na Peter Edibi wa Nigeria, wakati refa wa akiba atakuwa Mohamadou Mal Souley pia wa Cameroon.

Timu hizo zitarudiana Oktoba 19, Uwanja wa Mazembe mjini Lubumbashi, zikichezeshwa na marefa Haimoudi Djamel wa Algeria atakayesaidiwa na Achik Redouane wa Morocco na Etchiali Abdelhak wa Algeria, wakati refa wa akiba atakuwa Bousseter Sofiane  wa Algeria pia.

Mazembe inayoongozwa na washambuliaji wawili wa Kitanzania, Mbwana Ally Samatta na Thomas Emmanuel Ulimwengu, ikifanikiwa kuitoa Stade Malien itamenyana na mshindi wa Nusu nyingine, kati ya timu za Tunisia tupu, Club Africaine na C.S. Sfaxien.

Ikumbukwe Mazembe iliangukia kwenye Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini katika 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu na sasa inaelekea kufuta machungu kwa kutwaa taji hilo la pili kwa ukubwa kwa michuano ya klabu Afrika.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA