TFF YAZITUHUMU YANGA, MBEYA CITY KUENDEKEZA USHIRIKINA
Vitendo vivyoashiria imani za kishirikina ambavyo vilidaiwa kujitokeza katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Mbeya City dhidi ya Yanga, vimeziponza timu hizo.
Kabla ya kuanza kwa mechi hiyo iliyopigwa Jumamosi katika dimba la Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, yaliokotwa mayai katikati ya uwanja na kisha kukabidhiwa kwa meneja wa uwanja huo, Modestus Mwaluka.
Akizungumza katika mahojiano maalum jijini Dar es Salaam jana, Afisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Boniface Wambura (Pichani) , alisema wameshaikabidhi ripoti ya kamishna na ya waamuzi kwa kamati husika kwa ajili ya kuchukua hatua zaidi.
"Kwa sasa sekretarieti ya TFF haiwezi kuzungumzia suala hilo kwa sababu bado halijapitiwa na kamati husika. Tumepokea ripoti za waamuzi na kamishna wa mechi na kuikabidhi kwa kamati husika," alisema Wambura.
"Tukio hilo liko chini ya TFF kwa sababu ndiyo inayohusika na mambo yote yanayojitokeza ndani ya uwanja.
"Tusubiri maamuzi ya kamati husika. Wao ndio wataamua kulingana na kilichomo kwenye ripoti za maafisa wa TFF waliokuwa wametumwa kusimamia mechi hiyo," alisisitiza Wambura huku akikataa kubainisha timu itakayokumbwa na rungu hilo.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 32(1) ya Ligi ya TFF, inakataza klabu kujihusisha na vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina.
"Klabu ina wajibu na jukumu la kuhakikisha kuwa wachezaji, viongozi, wanachama na wapenzi wake wanajiheshimu na hawajihusishi na vitendo vyovyote vya utovu wa nidhamu kama vile matusi, vitisho, vurugu, vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina na vitendo vyovyote vingine visivyokuwa vya kimichezo," inaeleza kanuni hiyo.
Kanuni hiyo inaendelea kuainisha kuwa: "Klabu ambayo mashabiki wake watafanya vitendo hivyo, itatozwa faini ya Sh. 500,000 huku shabiki atakayethibitika kujihusisha na vitendo hivyo, akifungiwa kuingia uwanjani kwa kipindi kisichopungua miezi mitatu na kisichozidi mwaka mmoja."
Wakati Yanga na Mbeya City zikisubiri kamati ikae kutoa maamuzi, Klabu ya Simba imeponea chupuchupu kukumbana kuingia katika mkumbo huo, kwani nayo ilidaiwa kufanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina katika mechi yao ya pili ya ligi hiyo ambayo walishinda 1-0 dhidi ya Oljoro JKT kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Agosti 28, kabla ya kuanza kwa mechi hiyo iliyokuwa ya kwanza kwa Simba kupata ushindi msimu huu baada ya kushikwa kwa sare ya 2-2 dhidi ya Rhino Rangers mjini Tabora, ilidaiwa walimwaga maji yenye rangi nyekundu chini ya mlango wa basi lao wakati wachezaji wao walipokuwa wakishuka kuingia kwenye vyumba vya kubadilishia nguo.
"Kamati inatolea maamuzi mambo ambayo yamo kwenye ripoti za kamishna na marefa tu. Tukio la ushirikina linalodaiwa kufanywa na Simba jijini Arusha halikuwamo kwenye ripoti zao. Kamati haiwezi kukaa kuzungumzia suala ambalo halina ushahidi," alisema Wambura.
Rufaa ya Yanga yatupwa
Katika hatua nyingine, TFF imeitupilia mbali rufani iliyowasilishwa na Yanga kuomba kurudiwa kwa mechi yao dhidi ya Mbeya City kwa madai ya kujitokeza kwa vurugu uwanjani.
Jumapili uongozi wa Klabu ya Yanga ulisema umewasilisha rufaa TFF kwa njia ya barua pepe kwa Katibu Mkuu wa shirikisho hilo, Angetile Osiah kuomba mechi hiyo irudiwe katika uwanja huru kutokana na vurugu zilizotokea kabla ya mechi hiyo.
"TFF inashughulikia matukio ambayo yanatokea ndani ya uwanja tu. Vurugu za mashabiki nje ya uwanja na suala la magari ya Yanga kupigwa mawe ni ya polisi, hatuwezi kuita kamati kuzungumzia mambo ambayo hayapo.