TAMBWE AZIDI KUTIKISA LIGI KUU

Mshambuliaji Amisi Tambwe (Pichani) jana alifunga goli lake la saba katika mechi tatu wakati alipoiongoza Simba kushinda 2-0 dhidi ya JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.


Tambwe ambaye amejiunga na Simba katika kipindi kilichoisha cha usajili akitokea kuipa ubingwa wa Kombe la Kagame la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati timu ya Vital'O ya kwao Burundi, alifunga goli la kuongoza katika ya dakika 25 kwa penalti.

Simba ilipata penalti hiyo baada ya beki wa kati wa JKT Ruvu, Omar Mtaki kuonekana ameunawa mpira wa krosi iliyopigwa na haruna Chanongo. Refa wa kati hakuona kama kuna madhambi yamefanyika lakini mwamuzi wa pembeni John Kanyenye kuotoa Mbeya aliamua kuwa ni penalti.

Wachezaji wa JKT Ruvu waliilalamikia sana penalti hiyo huku mtunza vifaa wao, Selemani Oga, akiingia uwanjani kumzonga mwamuzi.

Hali hiyo iliendelea hata baada ya mechi hiyo kumalizika pale mchezaji Paul Ndauka alipoingia uwanjani kumzonga mwamuzi huyo ambaye alijaribu kumkwepa kwa kurudirudi nyuma.
Matokeo hayo yalidumu hadi wakati wa mapumziko.

Kipindi cha pili JKT Ruvu walirejea kwa kasi kwa nia ya kusawazisha goli hilo, lakini kushambulia mfululizo kuliwagharimu kwani walijikuta wakifungwa goli la pili kwa shambulizi la kustukiza.

Kiungo Abdulhalim Homoud alikimbia na mpira kutokea katikati ya uwanja kabla ya kupiga krosi iliyomkuta Ramadhan Singano 'Messi' aliyeusukumia mpira wavuni kwa mguu wa kulia, ikiwa ni dakika sita tu baada ya mapumziko. Messi alikuwa ameingia uwanjani katika dakika ya 36 kuchukua nafasi ya Amri Kiemba.

Kwa ushindi huo, Simba imefikisha pointi 14 kileleni baada ya mechi saba.

Katika mechi nyingine, Azam FC iling'ang'aniwa kwa sare ya 1-1 dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya. Wenyeji Prisons walitangulia kupata goli katika dakika ya 36 lililofungwa na Peter Michael kabla ya Azam kusawazisha kupitia kwa Kipre Tchetche katika dakika ya 49.

Kwenye Uwanja wa Azam Complex, timu inayoburuta mkia ya Ashanti United ilipata pointi yake ya pili tangu irejee kwenye Ligi Kuu msimu huu baada ya kulazimisha sare ya 2-2 dhidi ya Mtibwa Sugar. Ashanti ilipata magoli yake kupitia kwa Paul Maone na Tumba Swedi, wakati ya Mtibwa yalifungwa na Shaaban Kisiga.

Vikosi kwenye Uwanja wa Taifa vilikuwa; Simba: Abbel Dhaira, Haruna Shamte, Adeyoum Seif, Kaze Gilbert, Joseph Owino, Abdulhalim Humoud, Amri Kiemba/ Ramadhani Singano (dk. 36), Said Ndemla, Betram Mombeki/ Miraj Madenge (dk. 73), Amisi Tambwe na Haroun Chanongo/Marcel Kaeza (dk. 57).

JKT Ruvu: Shaaban Dihile, Damas Makwaya, Stanley Nkomola, Omar Mtaki, Jamal Said, Nashon Naftali, Alhaj Zege, Emanuel Swita/ Richard Msenya (dk. 58), Bakari Kondo/ Paul Ndauka (dk.78), Salum Machaku na Emmanuel Pius.

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

HISTORIA YA TIMU YA MASHUJAA YA KIGOMA, KUMBE NI SHEA YA JESHI NA WANANCHI

STAA WETU: JEREMIA JUMA MTOTO WA JUMA MGUNDA ALIYEIKACHA SIMBA NA KUENDELEA NA UASKARI

MAKALA: SIMBA NI TIMU YA KWANZA TANZANIA KUINGIA NUSU FAINALI AFRIKA